Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC aona fursa mauzo ya ufuta ughaibuni

Chikki Til2 DC aona fursa mauzo ya ufuta ughaibuni

Fri, 5 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKUU wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Mwanahamisi Munkunda, amesema umefika wakati serikali kuanza kusafirisha na kuuza nje ya nchi ufuta, ili kuliongeza taifa fedha za kigeni.

Mkunda aliyasema hayo jana jijini hapa alipozungumzia umuhimu wa mfumo wa uuzaji wa mazao kwa njia ya stakabadhi ghalani.

Alisema Tanzania imekuwa mzalishaji mkubwa wa zao la ufuta kulinganisha na mataifa ambayo yanaonekana kuongoza katika usafirishaji wa zao hilo nje ya nchi.

“Tanzania tunaongoza kwa kuwa 'producer' (mzalishaji), lakini siyo 'exporter' (msafirishaji nje ya nchi) na mataifa ambayo mengine hata hayalimi zao la ufuta kama vile Kenya, 'wana-export' kuliko sisi. Sasa ipo haja ya kutafuta namna ya kusafirisha zao hili nje ili kupata fedha za kigeni,” alisema.

Alisema kinachotakiwa katika zao hilo ni kuboreshwa usafishaji na ufungashaji kwa njia bora na za kisasa.

Kiongozi huyo wa wilaya alibainisha kuwa katika kipindi hiki cha mavuno, Bahi imepata tani 400,000 za ufuta, ambazo kama zingesafirishwa na kuuzwa nje ya nchi moja kwa moja, zingekuza uchumi wa eneo hilo na kulipatia taifa fedha za kigeni.

“Nchi ambazo hivi sasa zinaongoza kwa uuzaji nje zao hili ni India ambayo na wao pia wananunua hapa kwetu, Ethiopia pia ambao wao katika uzalishaji wanatufutia na Nigeria, hawa ndiyo wanaongoza kwa sasa katika usafirishaji wa ufuta nje,” alifafanua.

Munkunda, akizungumzia mfumo wa uuzaji mazao kwa stakabadhi ghalani, alisema utawasaidia wakulima kunufaika na kilimo chao.

Alisema mfumo huo utawadhibiti walanguzi ambao walikuwa wananunua mazao kwa kujipangia bei na kwa vipimo visivyo sahihi.

“Mfumo huu ndiyo utakaomkomboa mkulima na kunufainika na kilimo chake, kwani mkulima atakuwa na sauti ya kupanga bei sahihi iliyopo sokoni na kutumia vipimo sahihi tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo wanunuzi walikuwa wanajipangia bei,” alisema.

Akizungumzia hali ya chakula katika wilaya yake, kiongozi huyo alisema kuwa kipo cha kutoa kutokana na wakulima kupata mazao mengi msimu huu wa kilimo.

Vilevile, alibainisha kuwa katika kuhifadhi mazingira, kipindi cha msimu wa mvua, wilaya hiyo imepanda miti takribani 150,000.“Lakini pia tumeagiza kila kaya ni lazima kupanda miti isiyopungua miwili, ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live