Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Tarime: Wafanyabiashara jitokezeni kupata elimu ya kodi

Dc Mara DC akizungumza na uongozi wa TRA

Tue, 8 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara Kanali Michael Mntenjele amewataka wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kwenye kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango inayofanyika wilayani humo ili waweze kutoa changamoto zao na kupata ufumbuzi.

Akizungumza na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaofanya kampeni hiyo ya elimu kwa mlipakodi wakati walipowasili wilayani humo, Mkuu wa Wilaya hiyo amesema kuwa, ni muhimu wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya kodi ili waweze kuelewa faida za kodi wanazolipa ndani ya nchi yao.

“Nitoe wito kwa wafanyabiashara wetu wa Tarime kama walipakodi wajitokeze kwa wingi na wawapokee waelimishaji wa TRA ili waweze kuwasilikiliza kwa lengo la kupata elimu ya umuhimu wa kulipa kodi kwasababu kodi hizo ndizo zinazoisaidia serikali kupata fedha kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa jamii”, alisema Mkuu huyo wa Wilaya ya Tarime.

Kwa upande wake mfanyabiashara wa nguo wa wilayani humo Zuhura Ally amesema kwamba, amefurahishwa na zoezi hilo ambapo amepata fursa ya kutoa changamoto zake ambazo zimefanyiwa kazi na maofisa hao wa TRA.

“Kwakweli ni jambo zuri TRA kujua wafanyabiashara tunaendeleaje na leo wameweza kutatua baadhi ya changamoto zangu na nyingine wameniambia nifike ofisini ili niweze kutatuliwa zaidi matatizo yangu,” alieleza Zuhura.

Nae mfanyabiashara wa mapambo ya magari wa wilayani humo Soti Warioba ameeleza kuwa, maofisa wa TRA wamebadilika sana tofauti na kipindi cha nyuma kiasi kwamba walipokuwa wanazunguka kwenye maduka mbalimbali kutoa elimu, hakuna mfanyabiashara aliyeogopa wala kufunga maduka.

Timu ya maofisa wanaofanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango mkoani Mara wako wilayani Tarime wakiendelea kutoa elimu ya kodi na baada ya wilaya hiyo wataelekea wilaya nyingine zilizopo ndani ya mkoa huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live