Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Singida awataka wawekezaji kuwekeza kwenye kilimo cha korosho

DC Sophia.png Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Sophia Kizigo.

Thu, 30 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Sophia Kizigo amewaalika wawekezaji kwenda kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo baada ya wilaya hiyo kuanza rasmi uzalishaji wa zao la korosho.

Alisema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa Dk.Binilith Mahenge pamoja na wataalam mbalimbali wa idara za Serikali.

Kizigo alisema wilaya hiyo ambayo awali ilikuwa ikitegemea mazao ya alizeti,vitunguu, dengu, pamba, mtama na mahindi kama mazao ya biashara sasa imeingia kwenye kilimo cha korosho ambapo imetenga ekari 200 kwa ajili ya kilimo cha korosho na kuwa msimu huu wa mazao ndio umekuwa wa kwanza kuvuna zao hilo.

“Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Korosho TARI Naliendele cha mkoani Mtwara walifanya majaribio ya utafiti wa ardhi kati ya Kongwa mkoani Dodoma na Singida kuona kama inaweza kuzalisha zao hilo”. Alisema Kizigo.

Alisema baada ya utafiti kubaini wilaya hiyo inafaa kwa kilimo cha korosho walitenga ekari 200 kwa ajili ya kilimo hichocha korosho na wananchi kuanza kukichangamkia ambapo alisema korosho hizo ni za ubora wa hali ya juu na ni tamu.

Kizigo alisema zao hilo litalimwa kila kata na watafanya programu maalum ya kuomba kukopeshwa mbegu ili wananchi wengi waweze kulima na kufundishwa namna ya kulima zao hilo ili waweze kupata fedha na kuweza kulipa kodi ambayo itaisaidia Serikali kujenga barabara, hospitali, shule na miundombinu mingine.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge alisema msimu huu wa kilimo Serikali itatoa mbegu bora za alizeti aina ya aisuni iliwakulima waweze kulima zaidi na zaidi ambapo aliwaomba wananchi wa wilaya hiyo kuchapa kazi kwa nguvu na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuliletea taifa maendeleo.

Alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya maajabu makubwa ya maendeleo ambapo kwa mwaka mmoja tu Mkoa wa Singida umepewa Sh.Bilioni 230 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo jambo ambalo lilikuwa halifanyiki kwa miaka ya nyuma.

Katika hatua nyingine Dk.Mahenge amepiga marufuku tabia ya baadhi ya walimu mkoani humo kuwarudisha wanafunzi nyumbani kwa sababu ya kushindwa kuchangia fedha za malipo kwa walimu wa kujitolea.

"Tunajua kuwa wapo walimu ambao wanajitolea ambao wazazi na walimu mlikubaliana kutoa mchango wa fedha za kuwawezesha mpaka hapo Serikali itakapoweza kupata walimu waajiriwa lakini kukosekana kwa fedha hizo isiwe sababu ya watoto kurudishwa nyumbani sitapenda kuona jambo hilo likitokea" alisema Mahenge.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mklama, Asia Mesos alisema wilaya hiyo walipokea zaidi ya Sh. 5 Bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikwemo ujenzi wa barabara, shule, vituo vya afya na Hospitali na maeneo mengine.

Katika mkutano huo watalaam wa idara zote za serikali waliweza kueleza kazi mbalimbali za miradi ya ya maendeleo zilizofanywa na Serikali na zinazoendelea kufanyika na kujibu kero zilizoibuliwa na wananchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live