Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC Mbulu afanya ziara ya kushtukiza mabuchani, vituo vya mafuta

10151 Mbulu+pic TZW

Thu, 28 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbulu. Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amefanya ziara ya kushtukiza kwenye vituo vya kuuza mafuta na mabucha ya nyama kwa lengo la kukagua bei elekezi ya serikali kama inatumika.

Mofuga alifanya ziara hiyo leo  Juni 27, akiambatana na Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na Ofisa biashara wa halmashauri ya mji wa Mbulu, Fortunatus Kalewa.

Mkuu huyo wa wilaya alikagua mabucha ya nyama kama bei elekezi ya Sh6,000 kwa kilo inafuatwa na uvaaji wa sare safi za uuzwaji nyama na utolewaji wa risiti za kielektroniki zinatolewa.

Amesema amebaini wauzaji wengi wa nyama hawavai sare maalum wakiwa kwenye mabucha yao na hawafanyi usafi wa kutosha na kutokutoa risiti kwa wanunuzi wa nyama.

"Ofisa biashara fungia bucha zote ambazo hazijakidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kutovaa sare, pia wanaouza kilo moja kwa zaidi ya Sh6,000 wanyang'anywe vibali vya kufanyia biashara," amesema Mofuga.

Pia, alibaini ubovu wa mashine ya kutolea risiti kwenye kituo kimoja cha mafuta na kumwagiza msimamizi wa kituo hicho kushughulikia tatizo hilo mara moja.

Ofisa biashara wa halmashauri ya mji wa Mbulu, Fortunatus Kalewa alimuhakikishia mkuu huyo wa wilaya kutekeleza agizo hilo kwa kuwachukulia hatua mabucha yote ambayo hayajatekeleza wajibu wao.

"Pamoja na hayo vituo vya mafuta ambavyo havina vifaa vya kuzimia moto (fire extinguisher) vilivyo bainishwa na kikosi cha zimamoto navyo vitachukuliwa hatua," alisema Kalewa.

Mkazi wa eneo hilo John Boay alipongeza hatua hiyo ya mkuu wa wilaya kufanya ziara za kushtukiza ili kuhakikisha maagizo aliyotoa kwa wafanyabiashara wanaouza nyama wameyatekeleza.

"Tunamshukuru mkuu wa wilaya kwa hili kwani awali hawa wenye mabucha walikuwa wanauza kilo moja ya nyama kwa Sh7,000, ila sasa hivi wanauza kilo moja sh6,000 tofauti na hapo awali." amesema Boay.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz