Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DART yaagizwa kutafuta mabasi ya Mbagala mapema

0c92ab2568b87b6dddeb795c1e5ab2a5 DART yaagizwa kutafuta mabasi ya Mbagala mapema

Wed, 19 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mhandisi Joseph Nyamhanga ameutaka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) kuandaa mapema utaratibu wa kumpata mtoa huduma ya mabasi yaendayo haraka katika barabara ya Kilwa.

Mhandisi Nyamhanga amesema ili kuwezesha utoaji huduma hiyo na mtoa huduma kamili, inabidi kuanza mapema hatua za manunuzi kabla ya ujenzi wa miundombinu ya awamu ya pili kukamilika

Aliyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo haraka Mbagala jijini Dar es Salaam.

“Mtendaji Mkuu nakuagiza wewe na timu yako mkae muone namna mtakavyotafuta mtoa huduma ya mabasi katika barabara hii ya Kilwa ili tatizo la kukamilika kwa miundombinu bila kuwa na mtoa huduma lisijitokeze tena kama ilivyokuwa kwa awamu ya kwanza ya mradi unaoanzia Kimara hadi Kivukoni, Moroco na Gerezani ambapo miundombinu ilikamilika lakini hakukuwa na mtoa huduma,” alisema Mhandisi Nyamhanga.

Alisema wakazi Mbagala na maeneo ya jirani wawe tayari kutumia fursa ya usafiri wa DART kwa vile serikali ipo katika hatua mbalimbali za kujenga miundombinu ya barabara za mabasi ya mwendokasi.

Alisema, miradi mikubwa ya kimkakati inalenga kuwaondolea kero Watanzania na kuinua uchumi wa nchi na kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

Akizungumzia maendeleo ya kujenga kituo kikuu cha Mbagala unaohusisha pia ujenzi wa karakana, Mhandisi Barakael Mmari amesema ujenzi umefikia asilimia 52.

Alisema kituo hicho kina uwezo wa kuegesha mabasi zaidi ya 400 na kitakuwa na majengo ya huduma za kijamii.

Alisema, usanifu na ujenzi wa eneo hilo umebadilisha uelekeo wa maji ambayo yalikuwa yaelekee kwenye makazi ya watu badala yake sasa yataelekezwa barabarani kwenye mfereji mkubwa ambao utayapeleka mtoni na hivyo kuepuka madhara ya kimazingira.

Mtendaji Mkuu wa DART, Mhandisi Ronald Lwakatare alisema, ujenzi wa miundombinu inayohusisha barabara, vituo mlisho, kituo kikuu na karakana ukikamilika watakua tayari kutoa huduma vizuri na wanajipanga kuanza kutoa huduma ujenzi ukikamilika.

Chanzo: habarileo.co.tz