Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Corona yapandisha bei mayai Dar

1b1f9ccb9a6c3ff337f4314a1860ab03.jpeg Corona yapandisha bei mayai Dar

Mon, 17 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

UGONJWA wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona umesababisha kupungua kwa mazao ya kuku na kupandisha bei ya mayai mkoani Dar es Salaam.

HabariLEO limebaini kuwapo uhaba wa mayai katika maeneo mengi ya Dar es Salaam, hivyo kusababisha trei moja la mayai ya kisasa kuuzwa kati ya Sh 8,000 hadi 10,000 kutoka wastani wa kati ya Sh 6,000 hadi 9,000.

Maeneo ambayo HabariLEO lilibaini ongezeko la bei ya mayai ni Kimara, Mbezi Luis, Kinyerezi, Goba, Ubungo, Sinza, Mwenge, Tazara, Ilala, Magomeni na Msasani.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga, alisema ni kweli mayai yameadimika kutokana na sababu mbalimbali ukiwemo mlipuko wa Covid-19.

“Katika rekodi zetu, Februari, Machi na Aprili mwaka jana shughuli za kitaifa na kimataifa zilisimama, ndege na meli zilisimamisha usafirishaji sababu ya ‘lockdown’ (kufungiwa) kwa baadhi ya nchi, uzalishaji wa kuku ukapungua kwa kuwa nasi tunaagiza pia mayai kutoka nje,” alisema Profesa Nonga.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni Watanzania kutochangamkia soko la ndani kutokana na sababu kadhaa ikiwemo ya kukatishwa tamaa na uchache wa watu wanaokula mayai.

“Hizo chipsi na mayai ya kisasa tunayokula mtaani yanategemea kuku wazazi si kuku wa kienyeji (asili). Hivyo, vifaranga tunavyozungumzia hapa ni lazima vitokane na kuku wazazi ambao wazalishaji wake walitikiswa na corona na kupunguza uzalishaji huku wengine wakisitisha kabisa maana soko liliyumba,” alisema Profesa Nonga.

Alisema mbali na Covid-19 kutikisa sekta hiyo mwaka jana na mwaka huu, uzalishaji wa mayai na utotoleshaji wa vifaranga unategemea zaidi kuku wazazi waliopo kwenye mashamba 28 pekee nchini yanayofanya idadi ya kuku wazazi milioni 1.3.

Alitaja mikoa yenye mashamba hayo na idadi yake kwenye mabano kuwa ni Dar es Salaam (9), Iringa (2), Njombe (1), Pwani (11), Kilimanjaro (2), Arusha (1), Mbeya (1) na Mwanza (1) na mashamba hayo ndio yenye kuku wazazi milioni 1.3.

Alisema idadi hiyo bado ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020/2021, Tanzania kuna kuku zaidi ya milioni 89, wa kisasa ni milioni 49.5 na wa kienyeji (asili) ni milioni 40.36.

Profesa Nonga alisema uzalishaji wa mayai hadi wiki iliyopita uliongezeka na kufikia mayai bilioni 4.49 kutoka mayai bilioni 4.05 yaliozalishwa mwaka 2019/2020 hali iliyotokana na kurejea kwa uzalishaji baada ya baadhi ya nchi kufungua mipaka na ongezeko la wafugaji wadogo wa kuku wa kisasa.

Alitaja nchi ambazo soko lipo la mazao ya kuku kuwa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda na Kenya.

“Ulaji wa mayai bado ni mdogo na tunapaswa kuhamasisha jamii zaidi. Sasa hivi hapa nchini mtu anakula mayai 106 kwa mwaka ikilinganishwa na wastani wa mayai 300 kwa mwaka yanayoelekezwa na FAO, tupo chini ya kiwango. Na hayo 106 ukijumlisha utakuta tunakula mayai bilioni 6.36 kwa mwaka, hivyo tunaleta nje mayai bilioni 1.87,” alisema.

Akaongeza: “Tukisema tule kwa mujibu wa FAO, ni mayai bilioni 18 kwa mwaka, hivyo utaona itabidi tu ‘import’ (tuagize nje) mayai bilioni 13.51 ili tule wastani wa mayai 300 kwa mtu kwa mwaka.”

“Haya ni mayai ya kisasa ambayo ndio tunaingiza kwenye takwimu kwa sababu ya kienyeji si rahisi sana kupata takwimu kwa namna ya ufugaji ulivyo.”

Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonesha kuwa, mayai yaliyozalishwa nchini hadi Aprili mwaka huu ni bilioni 4.49, lakini yanahitajika mayai bilioni 18 kwa mwaka ili kufikia kiwango cha Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) cha kila mtu kula mayai 300 kwa mwaka.

Hivi sasa Watanzania wanakula mayai bilioni 6.36 kwa mwaka sawa na mayai 106 kwa kila mtu kwa mwaka ikiwa ni sawa na yai moja kwa wiki.

Idadi hii inafanya nchi iagize nje mayai bilioni 1.87 kutokana na kuzalisha bilioni 4.49.

Chanzo: www.habarileo.co.tz