Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Corona yapaisha bei ya tende

TENDE+PIC.png Corona yapaisha bei ya tende

Mon, 18 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

IMEELEZWA kuwa ugonjwa wa corona umesababisha bei ya tende kupanda, huku zikiadimika katika maeneo mengi ulimwenguni hususan kipindi cha mfungo wa Ramadhani.

Kufuatia hali hiyo, Taasisi ya Misaada ya Miraji Tanzania, imetoa msaada wa tani moja ya tende, kwa waumini wa dini ya kiislamu wasiojiweza ikiwamo wajane wa Mkoa wa Dodoma ili kukidhi mahitaji yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo mkoani humo, Athumani Hotty, alisema wameamua kugawa msaada huo kutokana na umuhimu wa tende katika mfungo huo.

Alisema kutokana na kuwa adimu, lakini pia zinapatikana kwa bei ya juu hali inayowawia vigumu watu wasiojiweza kununua.

“Sisi tumeona ipo haja ya kutoa msaada huu kwa makundi haya maalum, tende kwa waumini wa dini ya kiislamu tunaelekezwa kuwa kabla ya kufungua Muislamu anatakiwa afungue kwa kula tende kutoka na kuwa inavirutubisho vingi ambavyo vinamsadia mtu aliyefunga kwa siku nzima,” alisema Hotty.

Aidha, aliwataka waumini hao katika mfungo huo kuendelea kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na virusi vya corona.

“Katika maeneo yetu ya misikiti tunasisitiza waumini kuendelea kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya kwa kunawa mikono, kuvaa barakoa, lakini pia kutoshiriki katika mikusanyiko ambayo ni eneo hatari kwa virusi hivi vya corona,” alisema Hotty.

Pia alisema kupitia Baraza kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoa wa Dodoma, wamekuwa wakitoa semina kwa maimamu wa misikiti yote namna ya kujikinga na ugonjwa huo katika nyumba zao za ibada.

Vilevile, alisema pamoja na kutoa semina kwa Maimamu hao, pia wanatoa misaada ya vifaa vya kujikinga na maambukizo ya corona kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live