Dar es salaam. Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini (Sumatra) imeruhusu magari madogo ya abiria aina ya Coaster kubeba abiria kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam kwenda mikoani.
Uamuzi huo umefikiwa leo Jumapili Desemba 23, 2018 baada ya idadi kubwa ya abiria wanaosafiri kukosa usafiri.
Awali, Sumatra walitoa vibali kwa magari yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 40.
Akizungumza na Mwananchi kituoni hapo, mkurugenzi wa udhibiti wa barabara kutoka Sumatra, Johansen Kahatano amesema uamuzi wa kuruhusu magari hayo ni kuhakikisha abiria wote wanasafiri.
Amesema awali walikuwa wakitoa vibali kwa magari yanayobeba abiria kuanzia 40 kutokana na wingi wa watu lakini bado kuna umuhimu wa kuongeza gari nyingine.
"Tunataka abiria wote wasafiri, tutakagua coaster zote na kuhakikisha zinafungwa vifaa vya kufuatilia mwenendo wa gari," amesema Kahatano.
Naye mkuu wa ukaguzi kutoka jeshi la polisi, Ibrahim Samwix amesema wameanza kukagua magari hayo ili yaweze kubeba abiri wanaoenda mikoani.
Hadi ilipofika saa 5 asubuhi idadi kubwa ya abiria waliokosa usafiri ni wale wanaokwenda mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.