Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chuo cha IFM chazidiwa wanafunzi

Sat, 1 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kutokana na ufinyu wa miundombinu unaoikabili Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam, wanafunzi wamelazimika kugawanywa katika mikondo tofauti ili kuepuka mrundikano katika madarasa.

Hayo yamesemwa leo wakati wa mahafali ya 44 ya IFM ambapo jumla ya wahitimu 2,840 wametunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha IFM, Profesa Tadeo Satta amesema tangu kuanzishwa kwake imekuwa ngumu kuongeza majengo kutokana na ufinyu wa eneo na hata yale yaliyopo yanakabiliwa na uchakavu.

"Kutokana na kuwapo kwa mikondo mingi hata uhitaji wa wakufunzi kuwa mkubwa ili kuweka urahisi wa ufundishaji na hiyo yote ni kwa sababu 2017/2018 hatukutengewa fedha na Serikali ambayo ingeweza kutusaidia katika kupunguza changamoto mbalimbali," amesema Profesa Satta.

Amesema chuo hicho kimejipanga kwa ajili ya kuanzisha tawi jijini Dodoma ambapo tayari ekari 773 katika eneo la Nala na ekari 14 katika eneo la Njedengwa kutajengwa shule ya biashara.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji mbali na kuahidi kushughulikia baadhi ya changamoto za chuo hicho aliwapongeza kutokana na kuendelea kusimamia dhima ya kuanzishwa kwa kwake tofauti na ilivyo kwa vyuo vingine.

"Kuna vyuo vingi vilianzishwa lakini mwisho wa siku wakaanza kutoka nje ya lengo la uanzishwaji wake," amesema Dk Kijaji.



Chanzo: mwananchi.co.tz