Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chumvi ya Pemba yapenya masoko ya Ulaya, Canada

Istock Salt Chumvi ya Pemba yapenya masoko ya Ulaya, Canada

Tue, 2 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali, amesema chumvi inayozalishwa katika kisiwa cha Pemba imepata mafanikio na umaarufu kwa kuingia katika soko la Ulaya hadi Canada.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, Balozi Amina, alisema hiyo ni hatua nzuri kwa wajasiriamali wazalishaji wa chumvi kutoka katika kisiwa cha Pemba kwa kuonyesha ubunifu wa usarifu wa uzalishaji huo.

Alisema chumvi hiyo yenye madini jote imepenya katika soko la dunia baada ya kusarifiwa kwa kuingizwa kwa baadhi ya mazao ya viungo ambavyo ni sehemu ya tiba.

“Napenda kuwajulisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba tayari uzalishaji wa chumvi katika kisiwa cha Pemba kupitia Swahili Coast Salts umepata mafanikio makubwa na kuingia katika soko la Ulaya,” alisema.

Aliupongeza uongozi wa kampuni ya Swahili Coast Salts chini ya mwekezaji wake, Stephanie Said, kwa kuonyesha uwezo wa ubunifu wa uzalishaji chumvi bora na kuingia katika ushindani wa soko la kimataifa.

Alisema mikakati ya Wizara ya Biashara ni kuimarisha sekta ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali kuanzia vidogo vya wajasiriamali hadi viwanda vikubwa na hivyo kuongeza pato la taifa.

Alisema tayari vipo jumla ya viwanda saba ambavyo vimeanzishwa na wajasiriamali wazalendo katika mwaka 2019-2020, huku vikianza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali na kuingia sokoni.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawapongeza kwa dhati wawekezaji wazalendo kwa uwekezaji wao katika sekta ya viwanda vidogo vidogo, hivyo kuzalisha bidhaa mbalimbali na kusaidia kutoa ajira kwa wananchi,” alisema.

Alisema Serikali ya Zanzibar imetenga jumla ya Sh. bilioni 6.85 kupitia kwa Wakala wa Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SMIDA) kwa ajili ya kukuza viwanda na maendeleo ya wajasiriamali kupiga hatua kubwa ya sekta ya viwanda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live