Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Choteni ujuzi kwenye maonesho ya Afrika Mashariki’

Maonesho Pic ‘Choteni ujuzi kwenye maonesho ya Afrika Mashariki’

Tue, 29 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imewataka wafanyabiashara na wajasiriamali wa Tanzania kuyatumia vyema maonesho ya 18 ya biahara ya Afrika Mashariki kwa kuchota ujuzi wa masoko, uzalishaji bora wa bidhaa na kutengeneza mahusiano ya kibiashara ili kukuza masoko yatakayokuza uchumi wa taifa unaotokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Akifungua maonesho hayo Agosti 28, 2023 katika uwanja wa furahisha jijini Mwanza; Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema yana umuhimu mkubwa kwa wafanyabiashara wa nchi washiriki kwani yanatoa nafasi kwa kampuni za ndani na nje ya nchi kutumia fursa ya soko la pamoja kujitangaza na kukuza soko la bidhaa zao.

Katika maonesho hayo yenye kaulimbiu ‘Mazingira Bora ya biashara ni kivutio cha kukuza uwekezaji wa biashara, viwanda na kilimo Afrika Mashariki', Kigahe amewataka waandaji kushirikiana vyema na mkoa, wizara na taasisi zinazohusika kuyaboresha kila mwaka ili yafikie hadhi ya kimataifa, yawe endelevu na kuitangaza Mwanza na taifa kwa ujumla.

“Kuna washiriki hapa kutoka Syria, India na Misri ambao wamekuja kuonyesha bidhaa zao hii ni fursa kwetu, wana Mwanza na Watanzania tutumie fursa ya soko la pamoja la Afrika Mashariki kutangaza bidhaa zetu, kukuza uchumi wa mkoa wetu na kuwa kitovu cha biashara kwa kukaribisha wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kutoka ukanda wetu,”

“Maonesho haya yanaweza kutumika kuimarisha mahusiano ya wafanyabiashara kwa kubadilishana ujuzi, uzoefu na kukuza mtandao wa wafanyabiashara na kuleta manufaa kwao. Pia kujifunza mbinu mbalimbali za kukuza soko la bidhaa kwenye maeneo mbalimbali, ni jukumu letu kuchangamkia fursa hizi na kupanua wigo wa uwekezaji, biashara na uchumi,”amesema Naibu Waziri Kigahe

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara na wenye Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Chacha amewahimiza wananchi kujitokeza kupata bidhaa za bei nafuu, elimu na ujuzi wa biashara, masoko na kujionea shughuli za utalii, vyakula vya asili na huduma muhimu huku, akiwakaribisha tena mwakani Agosti, 30 kwa maonesho mengine yatakayofanyika jijini hapa.

“Maonesho haya yalianza mwaka 2006 na mpaka sasa tunakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya uwanja wa kufanyia maonyesho, tunaomba wageni wanaokuja kutoka nje ya nchi wasaidiwe kuvuka mipakani kwa haraka pia ratiba za tarehe za maonyesho zimekuwa zikipangwa kwa kukaribiana na kuleta usumbufu kwa wageni kushiriki,” amesema Chacha

Mmoja wa washiriki, Gloria Mbilimonywa kutoka Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (Brela) amesema kutokana na ukuaji wa biashara na viwanda katika Jiji la Mwanza kupitia maonesho haya wanatoa huduma za papo kwa hapo za usajili wa biashara, leseni, viwanda, alama za biashara pamoja na kuendelea kuboresha huduma zao ziwe rafiki na gharama nafuu.

Naye, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda amesema Serikali ya mkoa huo itaendelea kushirikiana na jumuia ya wafanyabiashara kuhakikisha wanaboresha mazingira ya biashara.

“Mkoa wetu ni wa kimkakati kwahiyo tunahakikisha kuwa mazingira ya biashara yanakuwa rafiki na salama kwa wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza,”amesema

Chanzo: www.tanzaniaweb.live