Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo atoa maagizo kwa wachimba madini

C0bbb7068d3660b5b13af15b9bfdcf0e.jpeg Chongolo atoa maagizo kwa wachimba madini

Mon, 30 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewataka wachimbaji wadogo wa madini wilayani Shinyanga walinde miundombinu ya maji katika maeneo yao ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama. Alitoa rai hiyo jana wakati akikagua ujenzi wa tangi la maji la ujazo wa lita 500,000 lililojengwa katika Kijiji cha Mwakitolyo, mkoani Shinyanga.

Serikali inatumia Sh milioni 394.13 kujenga tangi hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 98 na unatarajiwa kukamilika mwezi ujao na litanufaisha wananchi zaidi ya 14, 600 katika kijiji hicho. Chongolo alisema mradi huo unatekelezwa kwa gharama kubwa, hivyo wachimbaji hao wadogo ni lazima wailinde miundombinu ya maji na wasikate mabomba ya maji yanayoendelea kusambazwa kwenye eneo hilo.

“Mradi huu ni fedha za wananchi, serikali inautekeleza kwa gharama kubwa na hapa Mwakitolyo ni kijiji cha wachimbaji madini, sasa niwaase msikate mabomba ya maji kwenye shughuli zenu za uchimbaji, mkiharibu miundombinu hii mnaharibu fedha za maendeleo kwa wananchi,” alisema.

Pia aliwataka wachimbaji hao watumie fursa waliyopewa na serikali ya kutenga maeneo ya wachimbaji wadogo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji ili nao wapate fedha na kuinua uchumi wao. “Serikali inawapenda, imewatengea maeneo ya uchimbaji mdogo na inawaletea miradi ya maendeleo kama hii ya maji, sasa niwatake tumieni fursa hii vizuri, fedha mnazopata zitumieni kuleta maendeleo yenu na sio kuzitapanya,” alisema.

Awali, akitoa taarifa ya mradi huo wa tangi la maji, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (Kashwasa), Patrick Nzamba alisema utakamilika Juni 2, mwaka huu. Alisema mradi huo umetekelezwa kwa awamu tatu na kwa sasa awamu mbili umefikia asilimia 98 na awamu ya tatu itakuwa ni usambazaji wa maji utakaotumia Sh milioni 615.3.

“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa tangi umekamilika kwa asilimia 98 , pia ujenzi wa uzio nao uko asilimia 90 awamu ya tatu ni Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Shinyanga (Ruwasa) wataanza kazi Julai Mosi, mwaka huu,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live