Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo aipa TBS siku saba kukagua kiwanda cha Kipanya

WhatsApp Image 2022 04 12 At 4.37.24 PM.jpeg Chongolo akizungumza na Masoud Kipanya

Wed, 13 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amelipa siku saba Shirika la Viwango nchini (TBS) kwenda katika kiwanda cha uzalishaji magari cha Ally Masoud almaarufu kama 'Masoud Kipanya' kwenda kufanya ukaguzi na vibali vinavyohitajika ili uzalishaji uanze mara moja.

Amesema atarudi ndani ya siku hizo akiwa na taasisi zote zinazohusika na udhibiti wa ubora ili kuharakisha mchakato wa kiwanda kuendelea.

Amesema uwezeshaji wa kiwanda ni jambo la muhimu kwa sababu linaongeza ajira kwa wananchi, kukuza teknolojia na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

“Ilani ya CCM iliahidi na imeendelea kuweka msukumo katika ubunifu, nitahakikisha wanathamini mchango wa wazalishaji wa ndani kikiwamo kiwanda hiki,” amesema.

Chongolo amemweleza Kipanya kuwa ahakikishe chama kinapata angalau gari moja ambalo litawekwa katika maonyesho na kutumiwa katika shughuli mbalimbali ili kuheshimu na kutangaza uzalishaji wa ndani unaofanywa na kiwanda hicho.

Amesema Kipanya kupitia kiwanda hicho ameweza kutengeneza gari linalotumia umeme ambalo kwa nchi siyo jambo dogo.

Chongolo amelipongeza Shirika la Kuhudumia Viwanda (SIDO) linalokuza ubunifu wa vijana nchini.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Kipanya amesema amekutana na matatizo mengi hadi sasa na ametumia zaidi ya Sh milioni 75 kwa uwekezaji wa awali na mahitaji yaliyopo ni kupata Sh. bilioni 2.5 kwa ajili ya kujenga kiwanda.

Amesema mchakato wa kuanzisha kiwanda hicho ulioanza mwaka 2013 na alisajili na kuanza uzalishaji wa kwanza mwaka 2020.

Meneja wa SIDO Mkoa wa Dar es Salaam, Ridhiwan Matanga amesema wameridhishwa na mwenendo wa kiwanda cha Kipanya ambaye baada ya kupata wazo alikwenda kwao na waliliboresha na hatimaye uzalishaji wenye tija umefanyika.

Amesema wameshirikiana na Kipanya ikiwamo kumpatia eneo la uzalishaji na kuahidi endapo atahitaji eneo kubwa zaidi SIDO watampatia ili aweze kujenga kiwanda kikubwa zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live