Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

China na mkakati mpya Bandari ya Bagamoyo

Bandari Bagamoyo China na mkakati mpya Bandari ya Bagamoyo

Fri, 29 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ubalozi wa China nchini umesema kuwa unajipanga kufaidika na mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Hatua ya ubalozi huo imekuja wakati Serikali ikirejea kwenye ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Akizungumza na wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara (TBNC) jijini Dar es Salaam Juni 26, Rais Samia Suluhu Hassan alisema wameanza mazungumzo ya kufufua mradi wa Bandari ya Bagamoyo pamoja na ule wa chuma na makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga.

Rais Samia alitoa kauli hiyo wakati kukiwa kumeibuka mjadala bungeni kuhusu bandari hiyo, ambapo aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai aliitaka Serikali kuangalia upya mradi wa bandari hiyo mkoani Pwani na iwapo ni jambo jema waendelee nao.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni, Balozi wa China nchini, Chen Mingjian alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi wanayoisubiri kwa hamu.

“Kwa sasa kampuni za China zinashiriki katika ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo reli ya kisasa ya kati na bwawa la Nyerere.

“Tunatarajia kwamba mamlaka za Tanzania na wawekezaji wa Tanzania watakuwa na majadiliano ya kina ya kuanzisha tena mradi wa Bandari ya Bagamoyo,” alisema Balozi Mingjian.

Mradi huo uliokuwa chini ya Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo (SEZ) ulizinduliwa rasmi na Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete mwaka 2015, ambapo Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya China Merchants Group, Dk Hu Jianhua na aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Usultani wa Oman Dk Ahmed Mohamed Al Furaisi walishiriki uzinduzi huo.

Pia ziara ya Rais wa China Xi Jinping nchini Tanzania Machi 2013, na kusaini mikataba 16 na mwenyeji wake Rais Kikwete kwa ajili ya kutia saini miradi ya maendeleo, ilitoa picha ya namna utawala wa awamu ya nne ulivyoamini kuhusu mradi huu wa Bagamoyo na faida zake.

Akisisitiza kuhusu mradi huo, Balozi Mingjian alisema, “Ni matumaini yetu kuwa China na Tanzania zitaungana na kufanya kazi pamoja, watafikia viwango vikubwa na matakwa ya hali ya juu, kujenga miradi mikubwa ya ushirikiano kati yetu na kukuza urafiki katika awamu mpya,” alisema.

“Tangu mwaka 1970, kampuni za China zimekuwa zikishiriki katika ujenzi wa miradi mingi ya kimkakati nchini Tanzania, kama vile reli ya Tanzania na Zambia ambayo imesimika urafiki kati yetu na Afrika kwa ujumla,” alisema.

Alimpongeza Rais Samia kwa kuiongoza Tanzania kuelekea kwenye maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii.

“Nchi zetu zinafanya kazi kwa pamoja katika mradi wa barabara (Belt and Road Initiative (BRI). Tutarithi na kupeleka mbele urafiki wetu wa jadi kwa kuwezesha kampuni za China kushiriki katika miradi mikubwa ya BRI.

Pia Balozi Mingjian alieleza kufurahishwa kwake na maboresho ya mazingira ya uwekezaji nchini.

“Rais Samia aliahidi kufanya mabadiliko kuimarisha mazingira ya uwekezaji mara alipochukua madaraka Machi 2021 na amejitanabaisha kuvutia wawekezaji kama kipaumbele chake.

“Nimejifunza kuwa Serikali ya Tanzania imefanya marekebisho ya sera ya uwekezaji na sheria ya kukuza uwekezaji. Mamlaka hizo zimewezesha kupunguzwa kwa gharama za kufanya biashara ikiwamo kupunguza kodi na mchakato wa kufanya kazi,” alisema.

Aligusia pia mchakato unaofanywa na Serikali kuanzisha Dirisha la Kielektroniki la Uwekezaji (TelW), ambalo wawekezaji watapata vibali kupitia kituo kimoja.

“Naamini maboresho hayo yatawavutia wawekezaji wengi wa kimataifa,” alisema.

Alitaja takwimu za kituo cha Uwekezaji (TIC), akisema China ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini.

“Wawekezaji wa China wameanzisha miradi katika sekta mbalimbali zikiwemo za usafirishaji, viwanda, uchimbaji madini, utalii, kilimo, uvuvi na viwanda.

“Miradi ya China inakadiriwa kuzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja za ndani zipatazo 150,000 zinazowezesha kuongeza mapato ya ndani.

Kuhusu mawasiliano ya simu, Balozi alisema kampuni za China zimejizatiti katika teknolojia ya kidigitali tangu miaka ya 2000.

“Natoa mfano wa kampuni ya Huawei. Kwa Tanzania ilianzishwa mwaka 2007. Kwa miaka 15 imepata watumiaji wengi wa bidhaa zake katika soko la mawasiliano ya simu na kuwa mshirika muhimu wa Serikali ya Tanzania na watoa huduma wa ndani,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live