Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Changamoto tatu zinazoua biashara zatajwa

Bei Za Bidhaaa Kupanda.jpeg Changamoto tatu zinazoua biashara zatajwa

Thu, 27 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Kuugua kwa muda mrefu, kupata ulemavu na kuzeeka ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuchangia kuua biashara za wajasiriamali wengi nchini.

Sababu hizo zimebainishwa leo Alhamisi, Aprili 26, 2023 na Mkuu wa Idara ya Biashara Benki ya NMB, Alex Mgeni katika kongamano lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Commmunications Limited (MCL) kwa lengo la kujadili namna ya kuwezesha biashara changa, za chini, ndogo na za kati (MSMEs) kukua haraka.

Kongamano hilo linafanyika katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki jijini Dar es Salaam limedhaminiwa na Benki ya CRDB, Kampuni ya usafirishaji ya DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media, Ashton na Ukumbi wa mikutano wa Dome.

Mgeni akitoa mada kuhusu mikakati ya kubadilisha uongozi na umiliki wa biashara, alisema ili kuhakikisha uendelevu kwa vizazi vijavyo ni lazima iwepo mikakati endelevu.

"Biashara tunazozianzisha lazima ziwe na maendeleo na warithi wanaoziendeleza. Jamii ya wenzetu Wahindi wamejitahidi sana kwenye kurithisha biashara zao.

"Changamoto hizo ni kuugua kwa muda mrefu ndiyo maana tunasisitiza kuna haja ya kuwa na mrithi zaidi ya wewe, pili unaweza kupata ulemavu lakini sababu ya tatu ni kuzeeka," amesema.

Mgeni amesema kutokuwa na mrithi husababisha mfanyabiashara kutokuwa na mwendelezo hasa katika mambo mapya na upya wa teknolojia.

"Kuna mauzo yanaweza kufanyika kwenye mtandao lakini ukiwa na kijana yeye ana muda wa kufanya tafiti na anaweza kutengeneza matangazo yanayovutia wewe hutaweza," amesema.

Ametaja kitu kingine kuwa ni uelewa wa mitaji ya biashara nafuu.

"Wapo watu wanapeleka watoto wao kusoma nje wanarudi na kuwaingiza kwenye biashara wanakuja na mbinu mpya, mfano kuna staili za batiki ambazo vijana wanapenda sasa wewe umezeeka hujui soko linahitaji nini...

"Ili kurithisha biashara ziwe endelevu kama huwa unafanya makubaliano ya kupunguza kodi na TRA mfundishe yule kijana wako namna ya kujadiliana punguzo ili afahamu hata siku usipokuwapo kwenye biashara awe na uwezo wa kuyafanya yote," amesisitiza.

Chanzo: mwanachidigital