Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Changamoto tatu zaukabili mfuko wa kukopesha wa ‘Self’

Selffff Selfff.png Changamoto tatu zaukabili mfuko wa kukopesha wa ‘Self’

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Changamoto tatu zimetajwa kuukabili Mfuko wa Self ulio chini ya Wizara ya Fedha, wakati unapotoa mikopo kwa wananchi wa kipato cha chini, ili waweze kujishughulisha na uzalishaji mali, kujiongezea kipato na kupunguza umasikini.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa mfuko huo, Mudith Cheyo, wananchi wamekosa uelewa wa kutosha wakati wa kufanya maamuzi ya kukopa au kutumia mikopo na kujikuta wakitumia pesa nje ya malengo yaliyokusudiwa.

“Wapo wanaokopa pesa kwa ajili ya biashara lakini anajikuta mambo yameingiliana na kutoa pesa hizo kufanyia shughuli nyingine. Akija kushtuka pesa zimeisha na hakuna alichofanyia,” amesema Cheyo.

Akizungumza katika kikao cha wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Machi 11, 2024, Cheyo amesema changamoto hizo ni wananchi kutokuwa na elimu ya fedha, urejeshwaji wa mikopo kwa hiari, huku akisema wengi wao hujishughulisha na biashara zisizo rasmi.

Amesema mfuko huo unatoa mkopo wa moja kwa moja kwa wakulima, wafugaji na vikundi pia unatoa mikopo katika taasisi ndogo za fedha zikiwemo saccos na watu wanaofanya biashara au kilimo.

Hata hivyo, Cheyo amesema hadi kufikia Desemba 31, 2023 mfuko huo umetoa mikopo ya Sh324 bilioni ikiwa na kiwango cha mikopo chechefu chini ya asilimia 10.

Cheyo amesema mikopo hiyo iliweza kuwafikia wanufaika wapatao 314,055 kati yao wanawake ni 166,449 sawa na asilimia 53, huku wanaume wakiwa 147606 sawa na asilimia 47 na wanufaika hao wakitoka katika mikoa 30 ya Bara na Visiwani.

Kufuatia mikopo hiyo, mfuko umetengeneza ajira 37,024 kwa mwaka 2023 kwa wakopaji na wale wanaoajiriwa na pia ulitoa elimu ya fedha kwa wakopaji 1,519.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mikopo wa Mfuko huo, Santiel Yona akiongezea suala la dhamana amesema, kikubwa wanachokiangalia katika ukopeshaji ni uwezo ambao wamefanyia tathimini ya biashara au taasisi katika kurejesha mkopo.

“Wakati mwingine tunaangalia tabia ya mtu kwenye marejesho ya biashara zake kupitia taasisi nyingine na tunazidi kuweka ushirikianao na wenzetu, lakini pia biashara ya mkopaji ina uwezo wa kurejesha marejesho kiasi gani,” amesema Santiel.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live