Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Changamoto sekta ya madini zaendelea kutatuliwa

Madini Pic Data Changamoto sekta ya madini zaendelea kutatuliwa

Tue, 13 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Tume kwa kushirikiana na Wizara ya Madini imeendelea kutatua changamoto katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini na kupeleka huduma ya umeme ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unaendelea kukua.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Februari 13, 2024 kwenye kikao cha Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma kilichoshirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Makamishna wa Tume, Wakurugenzi na Mameneja wa Tume chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo mwaka.

Amesema kuwa, pia Tume imeendelea kuhamasisha Taasisi za Kifedha kukopesha wachimbaji wadogo wa madini kupitia mikutano na majukwaa yaliyofanyika katika nyakati tofauti, kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu njia salama za uchimbaji wa madini pamoja na uboreshaji wa miundombinu hususan umeme ili uchimbaji wa madini uwe na tija.

Katika hatua nyingine amesema kuwa, Tume imeendelea kufanya kaguzi kwenye migodi mikubwa na midogo ya madini na kutoa elimu kuhusu uchimbaji salama wa madini, kutatua migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini kupitia makongamano na maonesho yaliyofanyika ndani na nje ya nchi.

Aidha, Mhandisi Samamba amewataka wachimbaji wa madini nchini kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia Sheria na kanuni za madini zilizowekwa.

Awali akitoa taarifa ya leseni za madini zilizotolewa katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba, 2023, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Profesa Abdulkarim Mruma amesema kuwa kamati ilipokea maombi mapya ya leseni za madini 2,369 yakijumuisha 81 ya leseni za utafutaji wa madini, 18 ya leseni za uchimbaji wa kati na 2,080 ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini, 13 ya leseni za uchenjuaji wa madini na maombi 177 ya leseni za biashara ya madini ambapo baada ya kufanyika kwa uchambuzi, maombi yote yalipitishwa baada ya kukidhi vigezo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live