Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Changamkieni fursa mradi wa bomba la mafuta’

A9510606cead3ceb13b6e52fe8576178.jpeg Bomba la Mafuta

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAFANYABIASHARA mkoani Dodoma wametakiwa kuchangamkia fursa ya ujenzi wa mradi mkubwa wa bomba la mafuta utakaoanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.

Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima hadi Chongoleani mkoani Tanga ambalo ujenzi wake utaanza hivi karibuni, lina urefu wa kilometa 1,443 kati yake kilometa 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania.

Mkurungenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoani Dodoma, Idd Senge, alitoa mwito jijini Dodoma akiwalenga wafanyabiashara nchini wakiwemo wa Mkoa wa Dodoma.

Aliwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi wa bomba hilo.

Senge alisema bomba hilo linalopita katika baadhi ya wilaya mkoani Dodoma, litahitaji makandarasi na watoa huduma mbalimbali ambazo wafanyabiashara wa mkoa huo wanatakiwa kuzichangamkia ili zisaidie kuongeza uchumi wao na mkoa kwa jumla.

Alizitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na usambazaji wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya ujenzi wa bomba hilo litakalopita wilaya za Chemba na Kondoa.

“Fursa nyingine ni kazi ya kusafisha maeneo au mahali litakapopita bomba hilo la mafuta pamoja na usambazaji wa bidhaa kama mafuta na maji kwa wanaojenga bomba hilo,”alisema.

Nyingine kwa mujibu wa Senge ni pamoja na usambazaji wa vilipuzi kwa ajili upasuaji wa miamba na maji ya ujenzi wa bomba hilo kwa mkandarasi au watu wanaojenga hapo pamoja na usambazaji wa mafuta kwa ajili ya magari na mitambo ya ujenzi katika mradi.

“Fursa nyingine ni pamoja na utoaji wa huduma za chakula pamoja na usambazaji wa dawa kwa ajili ya huduma ya kwanza kwa wafanyakazi wa kampuni itakayokuwa inajenga mradi huo,” nchini.

Aliwataka wananchi wa kawaida kutozembea, kuchangamkia fursa hizo kwa sababu kuna kazi nyingi zitafanyika zitakazohitaji nguvu za wananchi wa eneo husika, hivyo wajiweke tayari.

Aidha, aliwaalika wafanyabiasha wa mkoani humo na wengine nchini kuhudhuria mkutano utakaowakutanisha wafanyabiashara na wakandarasi pamoja na mkandarasi mkuu wa mradi huo ambaye ni kampuni ya kimataifa ya Total.

Kwa mujibu wa Senge, mkandarasi huyo atakutana na makundi hayo Agosti 25, mwaka huu katika mkutano uliondaliwa na TCCIA na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Bomba hilo la mafuta ghafi litaanzia Hoima karibu na Ziwa Albert na kuvuka mpaka wa Uganda na Tanzania katika eneo la Masaka na kuingia Bukoba na kupita karibu na Ziwa Victoria nchini.

Litapita karibu eneo la Kahama mkoani Shinyanga, mkoani Singida, wilayani Kondoa na Chemba katika Mkoa wa Dodoma hadi Tanga. Kwa jumla litapita katika mikoa minane na katika wilaya 24 nchini.

Nchini Uganda, bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 296 sawa na asilimia 20.5 ya urefu wote wakati nchini Tanzania litakuwa na urefu wa kilometa 1,149 sawa na asilimia 79.5 ya urefu wa bomba hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz