Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema uboreshwaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ni wa muhimu na wenye tija na kwamba wananchi watarajie kushuka kwa bei za bidhaa zinazotoka nje.
Kwa mujibu wa Chalamila, wafanyabiashara walilazimika kupandisha bei za bidhaa kutokana gharama kubwa za usafirishaji walizokuwa wanaziingia na hivyo kuzifidia kwa mlaji.
Chalamila ametoa kauli hiyo ikiwa siku chache zimepita tangu Serikali itie saini mikataba mitatu ya uwekezaji katika bandari hiyo na kampuni ya DP World lengo, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa raslimali hiyo.
Kabla ya utiaji saini hiyo wawili hao, awali waliingia makubalino kuhusu uwekezaji huo (IGA), ulionekana kuleta sintofahamu kutokana na watu kuwa na maoni tofauti huku Serikali ikisema utakuwa na manufaa kwa nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 4, 2023; katika mkutano uliolenga kuelezea utekelezaji wa mipango ya Serikali, Chalamila amesema: “kama kitu walikuwa wananunua kwa Sh10, 000 basi watakipata kwa Sh6, 000.”
“...na Sh4, 000 itakuwa imeondolewa kama sehemu ya gharama aliyokuwa analipwa mwenye meli, kulingana na ufanisi wa sasa, huwezi kupakua mzigo kwa siku moja, ndiyo maana kuna msongamano unaowagharimu wenye mizigo kuwalipa gharama kubwa wenye meli.”
“Meli mnazoziona zimepaki kule kwa siku moja zinatozwa dola 35,000 sawa na Sh89 milioni na mwenye meli anakuambia umenikodi kuja kushusha mzigo na hujanikodi nije kusubiri kupakua mzigo,” amesema
Ametaja sababu za kwa nini meli zinashindwa kupakua mzigo haraka kwenye bandari hiyo kuwa ni kukosekana kwa maegesho ya meli na uchache wa vifaa vya kupakulia na kwamba vilivyopo vinatumia teknolojia ya zamani.
Amesema kitendo cha kuleta teknolojia mpya pamoja na kuongeza sehemu za maegesho ya meli, kutaleta matokeo chanya na kwamba “watu watakuwa wanapakua mzigo kwa siku moja na gharama za bidhaa zinazotoka nje hazitakuwa zinauzwa kwa bei ya juu,” amesema
Amesema kuna sehemu ya bandari hiyo ilikarabatiwa mwaka 2017/2018 na gharama yake ilikuwa si chini ya trilioni, ambazo ni nyingi na lengo lilikuwa ni kuongeza kina cha maji kutoka mita nane hadi 14 na kuongeza lango la bahari.
“Kununua vifaa vichache ikiwemo kifaa kinachoshika kasha kutoka kwenye meli na kurudisha nchi kavu na kifaa hicho kimoja ni Sh 35 bilioni na kwa Tanzania ili uwekeze kwenye bandari unahitaji kusahau kupeleka fedha shuleni, vituo vya afya ili tutengeneze tu bandari,” amesema
Amesema kama nchi, kujitosa kuendeleza bandari ni jambo ambalo haliwezekani ndiyo maana serikali ilikaribisha uwekezaji.
Katika maelezo yake ametolea mfano Kariakoo kuna waliouza maeneo yao na walioingia ubia na wawekezaji na wanaendelea kula kodi wote.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi amewashukuru wananchi kujitokeza kwa wingi kusikiliza taarifa za utekelezaji na utendaji wa serikali katika halmashauri zinazogusa maisha ya mwananchi.
“Wamegusia sekta zote muhimu za afya, elimu ya msingi na sekondari, barabara na madaraja yake, masoko, stendi na nyumba za watumishi wanaotoa huduma kwetu tunashukuru kwa hilo,” amesema.