Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CTI, wafanyabiashara wataka majadiliano mabadiliko ya kodi bajeti ijayo

9542 Cti+pic TZWeb

Wed, 20 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Arusha. Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) na wadau wa kodi jijini Arusha wameiomba Serikali kufanya marekebisho kwenye ukusanyaji wa baadhi ya kodi zilizobainishwa kwenye bajeti ijayo.

Mwenyekiti wa CTI, Dk Samwel Nyantahe alisema ongezeko la ushuru wa forodha kwenye uingizaji wa sukari ya nyumbani na mafuta ghafi linaweza kushusha uzalishaji wa bidhaa hizo nchini.

Alipokuwa akiwasilisha bajeti Alhamisi iliyopita, waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitangaza ongezeko la ushuru wa forodha katika uingizaji wa mafuta ghafi ya kula kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 huku ule wa sukari nao ukipanda kwa asilimia 15.

Hata hivyo, jana Nyantahe alisema ingawa ushuru huo umelenga kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza uzalishaji wa ndani, lakini unaweza kuwa na matokeo hasi kwa wawekezaji hasa wanaotegemea malighafi hizo.

“Sukari inategemewa sana katika uzalishaji wa bidhaa baridi pamoja na vitu mbalimbali, kodi ya uingizwaji wake inapoongezwa itawalazimu wawekezaji nao kuongeza bei kufidia gharama za uendeshaji,” alisema Dk Nyantahe.

Alisema CTI itaendelea kuzungumza na Serikali ili kupunguza gharama hizo ikiwamo kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na baadhi ya wizara.

Mkurugenzi mtendaji wa shirikisho hilo, Leodgar Tenga alisema bajeti imejibu kati ya asilimia 70 hadi 75 ya mambo waliyokuwa wakiyalalamikia miaka mingi jambo ambalo litawahamasisha wazalishaji.

Akizungumzia kusamehewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (Vat) kwenye vifungashio vya dawa, malighafi za vyakula vya mifugo na taulo za kike, Tenga alisema kutachangia kuongeza uzalishaji wa bidhaa hizo. “Jambo hili litachangia viwanda vyetu kuwa katika ushindani, kuchochea uanzishaji wa viwanda vya kutengeneza chakula cha mifugo na kuwafanya wanawake kuweza kumudu gharama za kununua taulo za kike,” alisema Tenga.

Wataka maboresho

Nao wadau na wataalamu wa kodi mkoani Arusha wametaka kufanywa maboresho katika mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali hasa mabadiliko ya kodi, tozo na ushuru uliotangazwa.

Wakizungumza katika semina iliyoandaliwa na Kampuni ya Claritas International jana, wafanyabiashara na wadau walisema bajeti ijayo itakuwa bora zaidi kama itaboreshwa.

Mtaalamu wa kodi wa Claritas, Angelica Tarimo alisema, “badala ya kusamehe Vat ielezwe kodi itakuwa asilimia sifuri, hivyo wenye viwanda nchini wataendelea kupata unafuu katika malighafi wanazotumia.”

Kuhusu mafuta ghafi yanayoingizwa kutoka nje, alisema nia ya kuwawezesha wakulima wa mazao yanayozalisha mafuta kupata soko ni njema, lakini ni jambo la muda mrefu kwa kuwa hakuna malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda nchini.

Mchumi na mtafiti mwandamizi, Dk Abel Kinyondo alisema sekta ya utalii ilipaswa kutengewa fedha nyingi zaidi ili kuboresha miundombinu na kutangaza vivutio nje ya nchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz