Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CRDB yawashukuru wateja kwa kutwaa tuzo ya Euromoney

2195eb9182ee32a5121d5eaf1ef25bbe.jpeg Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela

Sat, 23 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki ya CRDB imewashukuru wateja na wadau wake baada ya kutunukiwa tuzo ya “Benki Bora Tanzania” na jarida maarufu la masuala ya fedha na uchumi la Euromoney la nchini Uingereza.

Shukrani hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe wa bodi, wafanyakazi, na wateja, wa Benki hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam, Nsekela alisema wateja wa benki hiyo wamekuwa sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa mkakati wa mageuzi ya biashara ambao umepelekea kupata tuzo hiyo.

“Niwashukuru wateja, wanahisa, Serikali, Benki Kuu ya Tanzania na washirika wetu wa biashara kwa ushirikiano wanaotupa na kuendelea kutufanya kuwa bora zaidi. Hii sio tuzo ya Benki ya CRDB peke yake, ni tuzo ya Watanzania wote,” alisema Nsekela.

Mwaka 2019, Benki hiyo ilianza ikifanya mageuzi katika biashara yake ambayo yamejikita katika kutengeneza thamani endelevu, kuongeza ujumuishi wa kifedha, na kujenga uchumi jumuishi kupitia bidhaa, huduma, na mifumo bunifu ya utoaji huduma.

“Tuzo ya Euromoney inathibitisha nafasi ya Benki ya CRDB kama ‘Benki Kiongozi’ nchini. Vilevile, inatambua mafanikio ya mageuzi haya ambayo yamepelekea ukuaji endelevu wa Benki yetu na ukinufaisha wateja, wawekezaji na uchumi wa nchi kwa ujumla wake.

“Tumekuwa pia tukishiriki kikamilifu katika kusaidia sekta mbalimbali za maendeleo nchini hususani kilimo, na ujusariliamali ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa Benki hiyo ilitoa ahueni kubwa kwa sekta ya biashara nchini katika kipindi ambacho janga la UVIKO-19 limeikumba dunia.

Aidha, alisema Benki hiyo pia imetambuliwa kwa kuwa na uwezo mkubwa katika uwezeshaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali na sekta binafsi akitolea mfano Mradi wa Umeme wa Maji wa Nyerere na Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa jitihada na mafanikio hayo pia yamekuwa yakijidhihirisha katika matokeo ya kifedha ambayo imekuwa ikiyapata mwaka hadi mwaka.

Benki ya CRDB ndio Benki ya kwanza nchini kutunikiwa tuzo ya ‘Benki Bora Tanzania’ na Euromoney mwaka 2004.

Mwaka jana, Benki hiyo ilitajwa kama Benki Bora Tanzania’ na ‘Benki inayoongoza kwa Ubunifu’ na jarida maarufu duniani la masuala ya fedha la ‘Global Finance’, huku Taasisi ya Utafiti wa Ubora barani Ulaya ikiitunikia ‘Tuzo ya Ubora’.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live