Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CRDB yatangaza punguzo la riba kwa wakulima

CRDB CRDB yashusha riba hadi 9% kutoka 20%

Mon, 24 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki ya CRDB leo imetangaza punguzo kubwa la riba katika mikopo kwa kundi la wakulima, pamoja na wafanyakazi. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Makao Makuu ya benki hiyo yaliyopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema punguzo hilo la riba linakuja kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mabenki kuhusu kupunguza riba ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Nsekela amesema katika punguzo hilo, riba ya mikopo ya kilimo imepunguzwa hadi 9% kutoka 20% iliyokuwa ikitozwa hapo awali, huku riba ya mikopo ya wafanyakazi ikipunguzwa kutoka 16% hadi kufikia asilimia 13%. Punguzo hilo la riba, linatoa ahueni kwa wateja wa Benki ya CRDB kulipa mikopo yao kwa riba nafuu, viwango vya chini zaidi vya marejesho ya awali, pamoja na kupata wigo mpana wa kukopa. “Kwa ushirikiano mkubwa na Benki Kuu ya Tanzania ambae ndie msimamizi wa sekta ya benki nchini, mwishoni mwa mwaka jana tuliweza kukaa chini na kuanza utekelezaji wa mchakato wa kupitia upya riba za mikopo mbalimbali inayotolewa na Benki yetu na hivyo ninajivunia kuona leo hii tumekuja na suluhisho la kilio cha muda mrefu cha wateja wetu,” amesema Nsekela huku akiwahamasisha wateja na Watanzania kuchangamkia fursa hiyo.

Kwa upande wa mikopo ya kilimo Nsekela amesema punguzo hilo la hadi 9% ni kubwa kupata kutokea katika soko, huku akibainisha kuwa benki hiyo imetoa punguzo hilo ili kusaidia kuimarisha sekta ya kilimo ambayo huchangia 26% ya pato la Taifa na kutoa ajira kwa 75% ya Watanzania. “Lengo letu ni kuchochea kasi ya mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini kwa kuwawezesha wakulima wadogo na wakati kufanya kilimo cha kisasa kupitia mikopo nafuu ya pembejeo na zana za kilimo,” amesema Nsekela. Benki ya CRDB ndio inayoongoza nchini kwa kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo kwa kutoa asilimia 40 ya mikopo yote ya kilimo nchini. Punguzo hilo la riba katika mikopo ya kilimo inadhihirisha azma ya Benki hiyo katika kuunga juhudi za serikali za kuwaletea watanzania maendeleo kwa vitendo. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Benki ya CRDB imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi 1.6 trilioni kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani katika kilimo.

Akielezea punguzo la riba kwa mikopo ya wafanyakazi, Nsekela amesema benki hiyo imejipanga kuendelea kuboresha ustawi wa wafanyakazi nchini kupitia mikopo ya riba nafuu. “Wafanyakazi ni kundi muhimu kwa Benki yetu ndio maana tumekuwa tukiboresha kwenye riba ya mikopo ya kundi hili kila mwaka ili kuwasidia kufikia malengo waliyojiwekea jambo ambalo litaongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi,” amesema Nsekela.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live