Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CRDB yapata faida Sh104 bilioni mwaka 2018

40647 Crdb+pic CRDB yapata faida Sh104 bilioni mwaka 2018

Fri, 8 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Miezi mitatu baada ya Benki ya CRDB kubadili uongozi, imetangaza kupata faida ya zaidi ya Sh104 bilioni.

Mmkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela amesema faida hiyo imetokana na kuimarika kwa ufanisi.

Kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2018 benki hiyo imepata faida ya Sh104.77 bilioni kabla ya kodi ikilinganishwa na Sh46.94 bilioni ilizopata kipindi kama hicho mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 128.

"Tumefanikiwa kupata matokeo haya kutokana na kuzingatia mikakati tuliyojiwekea.  Tunao mkakati wa miaka mitano na matumizi makubwa ya teknolojia yamesaidia kwa kiasi kikubwa kutufikisha tulipo,” amesema Nsekela.

Ikiwa na mawakala 3,558 wa fahari huduma, vituo 900 vya huduma na mashine 551 zinazohudumiwa na matawi 265 yaliyopo nchini kote, mkurugenzi huyo alisema huduma bora wanazozitoa kwa wateja wao ni sehemu muhimu wanayoipa kipaumbele.

Kupatikana kwa faida faida hiyo, taarifa za fedha za CRDB zinaonyesha kumetokana na kupungua kwa mikopo isiyolipika kutoka Sh430.6 bilioni mpaka Sh281.6 bilioni huku uwiano wake na jumla ya mikopo yote iliyotolewa ukishuka kutoka asilimia 13.6 hadi 8.32 ndani ya mwaka mmoja.

Katika kipindi hicho, mali za benki hiyo zilizongezeka kwa asilimia 1.6 na kufika Sh5.9 trilioni huku amana za wateja nazo zikiongezeka kutoka Sh4.1 trilioni mpaka Sh4.8 trilioni.

Kwa takwimu hizo, benki hiyo imeanza kupata faida nono baada ya kupitia kipindi kigumu kilichosababishwa na kuyumba kwa sekta nzima ya fedha nchini.

Mwaka 2016, faida ilipungua mpaka Sh74.1 bilioni baada ya kodi kutoka Sh129 bilioni iliyopata mwaka uliotangulia. Hali ilikuwa hivyo mwaka 2017 ilipopata faida ya Sh30.8 bilioni baada ya kodi ambayo mwaka jana iliongezeka mpaka Sh70.18 bilioni.

“Tumejielekeza zaidi kwa wateja wadogo huku tukiendelea kuwahudumia vyema wale wakubwa. Huduma nyingi sasa hivi tunazitoa kwa mfumo wa dijitali, tumepunguza riba kwa wateja wa kawaida na wafanyakazi,” amesema Nsekela.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz