Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CRDB yaipiga jeki Benki ya Wananchi Tandahimba

9684 B+PIC TZWeb

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Benki ya CRDB imeipatia Benki ya Wananchi ya Tandahimba (Tanecu) mtaji wa Sh3.2 bilioni ili kuiongezea nguvu ya kujiendesha na kuhudumia wananchi.

Kuongezwa kwa mtaji huo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kuzitaka benki za Taifa kuwa na mtaji unaoanzia Sh15 bilioni huku benki za wananchi zikitakiwa kuwa na mtaji wa Sh2 bilioni.

Akizungumza katika utiliaji wa saini wa mkataba kati ya benki hizo, Mkurugenzi mtendaji wa CRDB, Charles Kimei alisema wanaamini kwa muda wa miaka miwili walioutaja watakuwa wamefanikiwa kupata pesa hiyo.

“Hata sisi tunaamini kwa miaka miwili tutakuwa tumefanikiwa kuiimarisha na kama mtaji utapungua tutaongeza ili kuhakikisha haifungwi na inazidi kutoa huduma kwa wananchi,” alisema Dk Kimei.

Alifafanua kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008 kwa mtaji mdogo wa Sh500 milioni ambao karibu wote uliishia katika utengenezaji wa mifumo ya kibenki na hadi wanaanza kutoa huduma ulikuwa umekaribia kuisha.

“Tangu kuanzishwa kwake walikuwa wakipata hasara tu ambayo ilifikia Sh1.5 bilioni 2015 jambo ambalo likawafanya kutafuta hatua ya kuinusuru badala ya kuifunga,” alisema Dk Kimei.

Alifafanua kuwa kutokana na jambo hilo, CRDB ilichukua jukumu la kuinusuru kama moja ya mikakati yao ya kuwafikishia wananchi huduma za kibenki.

“Mbali na kuwapa ukwasi wa kujiendesha pia 2017 mwanzoni tuliwapatia ‘management team’ ambayo ingeweza kuwasaidia katika uendeshaji wa benki hiyo.

“Tangu tumewapa uongozi mpya wakaanza kufanya biashara mabadiliko yakaanza kuonekana na kuamini kuwa benki hiyo inaweza kuwa kichocheo cha uchumi kwa Mkoa wa Mtwara na hasara waliyokuwa wakiipata ikaanza kupungua,” aliongeza.

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Kijamii Tandahimba (Tacoba) Rajab Mmunda alisema kwamba katika miezi 24 waliyopewa watahakikisha wanaongeza idadi ya wanunuaji wa hisa na kutengeneza mtaji wa kutosha.

Chanzo: mwananchi.co.tz