Dar es Salaam. Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) nchini Tanzania imezitaka kampuni za kimataifa zinazotekeleza miradi mikubwa ya ujenzi nchini humo kuzishirikisha kampuni za ndani.
Akizungumza leo Alhamisi Desemba 19, 2019 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Consolata Ngimbwa amesema kwa uhalisia uliopo sasa ushiriki wa kampuni za ndani uko chini sana.
Amesema hatua hiyo inaashiria kutakapokuwa na uhitaji wa marekebisho yoyote katika kazi zinazofanyika itawalazimu wataalam kutoka nje kuja kufanyia maboresho.
Ngimbwa ameyasema hayo wakati wa ziara ya viongozi wa bodi hiyo katika miradi mikubwa ya ujenzi inayotekelezwa jijini Dar es Salaam.
Amesema bodi hiyo imebaini hatua ya kukosekana kwa kampuni za ndani katika miradi hiyo kunarudisha nyuma jitihada za kuwakuza wakandarasi wazawa.
“Tumeona hiyo dosari na tunataka ifanyiwe kazi, sheria iko wazi ni muhimu kwa kampuni za ndani zishiriki ili zipate ujuzi ili hata baadaye tuanze kufanya kazi hizi wenyewe,” amesema
Ngimbwa amesema walipotaka kujua sababu za kampuni za ndani kutoshirikishwa wanaambiwa ni kampuni hizo kukosa vifaa jambo ambalo hawaoni kwamba ni kikwazo.
“Hizi kampuni za nje zinasema wanashindwa kushirikisha kampuni za ndani kwa sababu ya kukosa vifaa na mitambo. Bado hatuoni kama hiyo ni sababu wangeweza kuwachukua kama nguvu kazi wakajifunza kupitia mitambo yao,” amesema
Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kuzitaka kampuni za ndani kuunganisha nguvu na kushiriki kwenye miradi hiyo.