WAZIRI Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, ameishauri Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuweka utaratibu wa kufadhili tafiti zenye kupeleka teknolojia mpya kwa wakulima hususani katika kuongeza thamani na kupata soko sahihi.
Pinda amesema leo Agosti 7 baada ya kutembea banda la Tume hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale vilivyopo jijini Mbeya.
Pia ameishauri Tume hiyo kufikiria kuanzisha wiki ya matokeo ya tafiti zenye tija kwenye jamii kwa kushirikiana na Taasisi za Utafiti na Vyuo Vikuu, huku akiipongeza serikali kupitia COSTECH kwa kuendelea kufadhili Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), na Kituo cha Tengeru.