Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CMSA yatoa maagizo kwa Benki za biashara Tanzania

73084 Benki+pic

Tue, 27 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imezitaka Benki za biashara nchini Tanzania kuanzisha huduma ya Uhifadhi  na Usimamizi wa Dhamana na Uwekezaji katika masoko ya mitaji kwa lengo kuongeza idadi ya wawekezaji.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama alisema hayo jana Jumatatu Agosti 26,2019 wakati akizindua huduma ya Usimamizi wa Dhamana na Uwekezaji katika Benki ya I&M.

Mkama alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo itazisaidia benki hizo kuongeza idadi ya wawekezaji na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

“Kuzinduliwa kwa huduma  hii ya Usimamizi wa Dhamana na Uwekezaji (Custodial and Investment Management Services) kutawezesha na kurahisisha biashara kwa wawekezaji wa kigeni katika soko la hisa,” alisema Mkama..

Pamoja na mambo mengine, Mkama alitoa wito kwa benki hizo kutumia fursa zilizopo katika sekta ya masoko ya mitaji ikiwemo kuuza dhamana kwa umma na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam ili kuongeza mitaji yao.

"Hatua hii ni muhimu na itasaidia katika kutekeleza agizo la Serikali kwa benki zote za biashara pamoja na benki za wananchi kutimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji wa kutosha ili kuweza kujiendesha kibiashara," alisema Mkama

Pia Soma

“Pia kampuni za bima ni vizuri zikatumia  fursa zilizopo katika sekta ya masoko ya mitaji ili kuongeza mitaji yao. Jambo hilo litaziwezesha kampuni hizo kuwa na uwezo wa kushindana na zile za nje zinazotoa huduma ya bima hapa nchini.”

 Mtendaji huyo, aliitaka mifuko ya hifadhi za Jamii na taasisi za fedha kuunga mkono malengo ya Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda kupitia masoko ya mitaji nchini.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki I&M, Baseer Mohamed alisema benki hiyo inaendelea kukua kutoka kuwa taasisi ya fedha ya jumuiya hadi kuwa benki ya kibishara ambayo imesambaa ukanda wa Afrika Mashariki.

“Kuanzishwa kwa huduma hii kunakwenda kutanua wigo wa huduma zetu na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi, lakini pia huduma hii ni ushahidi tosha kuwa benki yetu itakuwa benki imara zaidi kwa wafanyabiashara wakubwa na wakati walipo Afrika Mashariki,” alisema Mohammed.

Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Benki ya I&M kutoka Kitengo cha Huduma ya Usimamizi wa Dhamana na Uwekezaji,  Frank Bunuma, alisema benki hiyo imeamua kuanzisha huduma hiyo kwa lengo la kuwasaidia wawekezaji katika kuwapa elimu juu ya namna na mahali pazuri pa  kuwekeza.

Bunuma alisema tangu benki hiyo iingie nchini mwaka 2010 hadi sasa imefanikiwa kuwa na matawi nane, katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Kilimanjaro.

"Tunatambua kuwa hii ni fursa nzuri kwa wawekezaji wa Tanzania kuwekeza katika masoko ya mitaji na dhamana ndani ya nchi pamoja na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, " alisema Bunuma.

Chanzo: mwananchi.co.tz