Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la utafiti la CIAT wamewasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa utafiti wa malisho yaliyoboreshwa uliotekelezwa kwa miaka minne katika kanda ya nyanda za juu kusini.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Dk Vincent Anney amezipongeza kwa hatua hiyo huku akitoa rai kwa watekelezaji wa matokeo ya utafiti huo kuhakikisha elimu na ujuzi uliopo kwenye taarifa unawafikia wafugaji wote nchini.
“Ili tuwe na ufugaji wenye tija ni lazima utafiti unaombatana na majaribio ufanyike kama ambavyo mradi huu umefanya kwa kushirikiana na Serikali hivyo nashauri iundwe kamati maalumu ya kufuatilia uendelezaji wa yote yaliyofanyika wakati wa mradi ili tutumie fursa tuliyoipata kusonga mbele badala ya kusubiri mradi mwingine” amesema Dk Anney.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI), Profesa Erick Komba amesema wamehitimisha mradi huo kwa mafanikio na kusema taasisi hiyo ipo tayari kushirikiana na wadau wenye lengo la kuendeleza sekta ya mifugo.
“Mbali na utafiti wa malisho, Taasisi yetu pia inafanya utafiti katika vyakula vya mifugo na ulishaje wake, Uzalishaji, uzazi, afya ya mifugo na haki za wanyama ambapo ili kutekeleza shughuli zake Taasisi yetu inapata fedha kutoka Serikalini, vyanzo vyetu vya ndani na kupitia wadau wa maendeleo kama CIAT na wengineo”amesema Prof Komba.
Naye Mwakilishi wa Shirika la CIAT, Dk An Notenbaert ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano waliouonesha wakati wote wa kutekeleza mradi huo ambao ulilenga kufanya utafiti wa malisho bora kwa mifugo na kuandaa taarifa ya utafiti itakayotumiwa na watekelezaji wa Sera katika kuinua sekta ya mifugo nchini.
Advertisement Kwa upande wa Mmoja wa wafugaji walionufaika kutokana na mradi huo kutoka mkoani Njombe, Juliana Mlagala amesema kuwa, malisho hayo yaliyoboreshwa yamewaongezea ari ya kuendelea kufuga baada ya kuonesha matokeo chanya kwenye mifugo yao.
Mradi wa Utafiti wa kilimo cha malisho yaliyoboreshwa bila kuathiri mazingira umetekelezwa na Shirika la kimataifa la Utafiti la CIAT kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Idara ya Mafunzo, Utafiti na Ugani kupitia taasisi yake ya TALIRI ambapo umetekelezwa kwa miaka 4 katika Halmashauri 3 ambazo ni Mufindi, Njombe na Rungwe.
Imeandikwa na
Happy Lazaro,Mbeya.
[email protected]