Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yawataka wafanyabiashara kuuza vyakula kwa bei elekezi

Mbeto Pic CCM yawataka wafanyabiashara kuuza vyakula kwa bei elekezi

Thu, 2 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, amewataka wafanyabiashara kushusha bei ya bidhaa ya vyakula na kufuata bei elekezi ya Serikali.

Amesema wananchi wengi wanashindwa kumudu gharama za chakula kutokana na bei kuwa juu huku kipato chao kikiwa cha kawaida.

Maelekezio hayo ameyatoa jana katika ziara yake ya kutembelea na kukagua maghala ya kuhifadhi bidhaa za chakula, na gati ya bandari ya kushusha makontena ya bidhaa hizo Malindi jijini Zanzibar.

Kupitia ziara hiyo pia ametoa wiki mbili kwa uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar, kuhakikisha wanamaliza tatizo la kushusha bidhaa za vyakula ili wananchi wapate huduma hiyo kwa wakati.

Amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea uhalisia wa sababu zinazokwamisha kupanda kwa bei za vyakula ambazo ni kinyume na bei elekezi ya Serikali.

“Licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiutendaji kwa upande wa bandari na wafanyabishara, bado sio kigezo cha kupandisha bei za vyakula kinyume na utaratibu uliowekwa na Serikali.

“Bidhaa zikishushwa kwa wingi zikaingia mitaani na bei isiposhuka basi tatizo litakuwa ni kwa wafanyabishara wanaodai kuwa mchele mwingi haujashushwa upo bandarini,”amesema Mbeto Khamis.

Pia ameonya kuwa, “ Tunazo taarifa za kuaminika kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanashusha bidhaa za vyakula katika bandari yetu ya Malindi kisha wanazisafirisha kwa njia ya magendo kuuza nje ya mipaka ya Zanzibar, wakati sisi chakula bado kinahitajika kwa wingi, wakikamatwa bidhaa hizo zitataifishwa na watachukuliwa hatua za kishria, amesema Mbeto.

Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana amekipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa maamuzi yake ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu juu ya tatizo la kupanda kwa bei ya vyakula Zanzibar.

Amewataka Wafanyabishara nchini kuhakikisha bidhaa za vyakula zikiwemo mchele, unga wa mahindi, mafuta ya kula, unga wa ngano na sukari vinapatikana kwa wingi mtaani na vinauzwa kwa bei iliyowekwa na Serikali.

Amesema Serikali imekuwa ikiweka mazingira rafiki kwa wafanyabisha kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila usumbufu, hivyo na wao wanatakiwa kuwa wazalendo ili wananchi waondokane na tatizo la kupanda kwa bei ya vyakula.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Nahaat Mohammed Mahfoudh, amesema wanaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha makontena yote yenye bidhaa za chakula yanashusha mizigo hiyo kwa wakati.

Ameeleza kuwa tayari wameshusha kontena 250 na zingine 250 zinaendelea kushushwa ili kuhakikisha bidhaa za vyakula zinachukuliwa na wafanyabishara kwa ajili ya kuingizwa sokoni.

Naye msimamizi wa ghala la kampuni ya Ever Green, Said Salum Khalfan, amesema katika ghala lake tayari kuna mchele tani 500 na nyingine inaendelea kushushwa bandarini. Amesema mchele huo wanauza mfuko mmoja wa kilo 50 kwa Sh82,600 na kilo 25 kwa Sh43,000 bei ambayo ni ya kawaida.

Juzi Rais Mwinyi, alizungumza na wafanyabisha wa bidhaa za vyakula na kuwataka kushusha bei, kwani wananchi wanaumia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live