Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yakemea urasimu ugawaji pembejeo za korosho

E98d7e1cea09ba38954238db45619b93 CCM yakemea urasimu ugawaji pembejeo za korosho

Fri, 3 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza Serikali ya Mkoa wa Mtwara iache urasimu kwa kuchelewesha ugawaji wa pembejeo kwa wakulima wa korosho.

Aidha, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka amemuagiza Mkuu wa Mkoa huo, Michael Gaguti aunde timu itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa huo kuchunguza sababu ya kukwama kwa baadhi ya miradi ya maji wilayani Nanyumbu.

Shaka alitoa maagizo hayo baada ya kuwasili mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi akitokea Lindi. Baada ya kufika Mtwara alisikiliza kero za wananchi ikiwemo ya baadhi ya vijiji kutopata pembejeo. Shaka aliiagiza Serikali ya Mkoa huo igawe pembejeo za kilimo kwa kuwa hakuna sababu ya kuzichelewesha wakati Rais Samia alishazitoa na zilishafika mkoani humo.

“Tumetoka asubuhi tumezungumza na Mkuu wa Mkoa taarifa ambayo nimepatiwa pembejeo zimeshafika, hivyo niwatake Serikali ya Mkoa wa Mtwara waache urasimu, ndani ya wiki moja pembejeo ziwe zimetoka, tunataka wananchi wanufaike na uwepo wa Rais Samia ambaye ameamua kutoa bure pembejeo za kilimo, lengo kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo chao,” alisema.

Shaka pia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara afanye uchunguzi kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama baada ya kubainika uwepo wa mradi wa maji Nandete unaosuasua wakati wananchi wakikabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji.

Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mnanje wilayani Nanyumbu, alisema ana taarifa za kutosha za mradi wa maji Nandete hivyo ametaka kupata majibu kabla ya kuondoka mkoani humo.

“Huu mradi wa maji Natende nataka majibu yake na Mkuu wa Mkoa tumia vyombo vyako kupata taarifa na bahati nzuri taarifa zote ninazo. Kuna mambo mengi yamefanyika na hawasemi, kuna mambo mengi yamejificha,” alisema Shaka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live