Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imewataka wakulima wanaopokea pembejeo za Serikali, kutoa taarifa iwapo hawatopata ujumbe mfupi wa simu (sms) unaoonyesha kiasi cha pembejeo alichopata kupitia vyama vya msingi vya ushirika (Amcos).
Aidha wakulima pia wametakiwa kuhakiki kiasi cha pembejeo wanachopokea kinalingana na kilichotajwa katika ujumbe huo mfupi wa simu.
Hayo yameelezwa Juni 27, 2023 na Mkurugenzi wa CBT kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, akiwataka wakulima ambao hawatapata ujumbe wa simu baada ya kupata pembejeo au changamoto yoyote ya ugawaji wa pembejeo, watoe taarifa bodi.
Katika msimu huu wa 2023/2024 pembejeo zinatolewa kwa wakulima kwa kuzingatia idadi ya miti iliyopo shambani vilevile mkulima anapatiwa viuatilifu vya aina tatu kwa wakati mmoja.
Viuatilifu hivyo ni kwa ajili ya kukinga, kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu wa mikorosho.
Pembejeo hizo zinatolewa kwa kutumia mfumo wa kidigitali kupitia namba maalumu ya utambulisho ambazo wakulima walipatiwa baada ya kusajiliwa.
Hivi karibuni waandishi wameshuhudia baadhi ya vyama vya msingi, (Amcos) katika Wilaya za Nanyumbu, Mtama na Ruangwa wakigawa pembejeo bila wakulima kupata mrejesho wa ujumbe mfupi katika simu zao
Baadhi ya wakulima walishangazwa na hali hiyo sababu walishaelezwa kuwa baada ya kupokea watapata ujumbe mfupi ukionyesha idadi ya pembejeo walizopokea.