Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CAMARTEC yajipanga kuongeza wigo soko la korosho

CAMARTEC CAMARTEC yajipanga kuongeza wigo soko la korosho

Thu, 30 May 2024 Chanzo: Nipashe

Serikali kupitia Taasisi ya zana za kilimo CAMARTEC imejipanga kuongeza wigo wa kuuza korosho ghafi nje ya nchi na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ili kujenga uchumi wa ndani unaotegemea viwanda ili kuongeza ajira kwa vijana na kuongeza malighafi kwa ajili ya viwanda vya ndani.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa kituo cha zana za kilimo na teknolojia (CAMARTEC) Mhandisi Pythias Ntella wakati akiongea na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma kwenye Maonesho ya Wiki ya Viwanda na Biashara Maonesho yaliyolenga kuonesha jinsi teknolojia na zana mbalimbali zinaweza kuboresha sekta ya kilimo nchini ambapo wakulima na wananchi kwa ujumla walipata nafasi ya kujifunza na kuelewa jinsi serikali inavyojizatiti kuboresha sekta hiyo muhimu.

Aliongeza kuwa maonesho hayo yamefanyika wakati ambapo Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ilikuwa ikijadiliwa bungeni, na yalitoa fursa kwa wabunge kujionea na kujifunza umuhimu wa zana za kisasa za kilimo.

Amebainisha kuwa Taasisi ya CAMARTEC imeonesha teknolojia mbalimbali, ikiwemo zana za kuandaa mashamba, kupanda mazao, kupura mazao, kuchakata malisho ya mifugo, teknolojia ya biogesi na majiko ya biogesi, pamoja na teknolojia za kubangua korosho.

Alifafanua kuwa teknolojia hizo zote zinalenga kuboresha mnyororo wa thamani katika kilimo, kuongeza tija na kupunguza matatizo yanazowakabili wakulima mashambani.

Mashine ya kupanda mbegu inayotumiwa na trekta ni kifaa kinachounganishwa na trekta na kinatumika kupanda mbegu shambani kwa haraka na kwa usahihi. Mashine hii inasaidia wakulima kupanda mbegu katika mstari uliopangwa vizuri na kwa umbali sawa, hivyo kupunguza kazi ya mikono na kuongeza ufanisi wa kilimo. "Tunataka kuona wakulima wetu wakipata zana bora kwa gharama nafuu," alisema Mkurugenzi wa CAMARTEC. "Hii itasaidia kuongeza uzalishaji na kupunguza matatizo yanayowakabili mashambani."

Akifungua maonyesho hayo Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji alisema uchumi wa taifa unabebwa na viwanda na biashara huku akisisitiza kuwa idadi kubwa ya walioajiriwa katika Sekta viwanda na biashara ni vijana.

Aliongezea kuwa wizara inaandaa mkakati wa biashara kidijitali ambao unalenga katika kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia teknolojia katika kufanya biashara na kuwataka wafanyabiashara wawe waaminifu kwa wateja wanapofanya biashara mtandaoni.

Chanzo: Nipashe