Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CAG ataja benki 4 za Serikali zinazojiendesha kwa hasara

51726 CAG+BENK+PIC

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amebaini benki nne za Serikali kati ya sita (asilimia 67) zilikuwa zikifanya biashara kwa hasara kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Benki hizo ni, Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Benki ya Biashara ya TIB, Benki ya Maendeleo ya TIB, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Benki ya Posta Tanzania (TPB) na Benki ya Twiga.

Amesema kutokana na kuendeesha biashara kwa hasara, ilipelekea TWB na Benki ya Twiga kuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na kuwa na kiwango cha chini cha mtaji kama inavyotakiwa na benki hiyo.

Pia, CAG amebaini kwamba Benki ya Maendeleo ya TIB ilifuta mikopo yenye thamani ya Sh3.69 bilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2017.

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa mashirika ya umma ya mwaka 2017/18, CAG pia amebaini kwamba uwiano wa mikopo chechefu ya benki tatu dhidi ya mikopo yote ya benki hizo umekuwa ukiongezeka zaidi ya kiwango kilichowekwa cha asilimia 11.7 pamoja na lengo la BoT la asilimia 5.

“Nilibaini Benki tano za Serikali zilikuwa na uwiano wa chini wa mtaji wa msingi na mtaji wa jumla ikilinganishwa na mali zinazoambatana na vihatarishi na mali zilizo katika hali hatarishi zilizo nje ya urari wa kimahesabu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2014 na mwongozo wa BoT wa Agosti 5, 2015,” amebainisha CAG kwenye ripoti hiyo.

NBS tegemezi

Pia, CAG amebaini kwamba kiwango kikubwa cha shughuli kuu zinazofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinafadhiliwa na wahisani, jambo ambalo linaweza kuathiri utendaji wa shughuli muhimu za ofisi hiyo.

Amesema katika kipindi cha mwaka wa ukaguzi 2017/18, taasisi hiyo ilikuwa na bajeti ya Sh1.64 bilioni ambazo imewezeshwa na Serikali kwa ajili ya kushughulikia masuala muhimu yahusuyo taasisi isipokuwa mishahara.

“Kiasi cha Sh. bilioni 13.84 kilifadhiliwa na Mradi wa Mpango Mkuu wa Kitakwimu Tanzania (TSMP) kwa ajili ya kutimiza majukumu muhimu ya NBS, ambapo pesa zinatoka kwa wabia wa maendeleo,” amesema na kupendekeza Serikali iongeze ruzuku ili taasisi hiyo  iweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.



Chanzo: mwananchi.co.tz