RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere imebaini kuna hundi zilizochacha zenye thamani ya Sh milioni 352.12.
“Hundi iliyochacha huwa haiwezi kulipwa na benki. Ukaguzi wangu ulibaini hundi zilizochacha zilizotolewa kwa waathirika wa miradi zenye thamani ya Sh. 352,128,273.60 katika miradi miwili ambayo ni mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato na mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mzunguko wa nje katika Jiji la Dodoma kwa Kiwango cha lami (112.3 Km),” amesema CAG Charled Kichere.
Kichere ameyabainisha hayo jijini Dodoma jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwasilisha taarifa za ukaguzi bungeni kwa hesabu za mwaka 2021/22.
Amesema, hali hiyo ilisababishwa na uwepo wa malalamiko na migogoro baina ya waathirika wa miradi ambayo ilisababisha kutochukua hundi hizo zilizoandikwa kwao kwa ajili ya malipo.
“Kwa upande mwingine, kulikuwa na mawasiliano yasioyoridhisha kati ya watendaji wa mradi na waathirika wa miradi kuhusu kuhamasisha uchukuaji wa hundi hizo za malipo.
“Ninaamini kuwa hundi zilizochacha zilisababisha fedha kurerejeshwa kwenye akaunti za benki za miradi, hivyo zinaweza kusababisha matumizi ya fedha hizo kwenye shughuli zisizopangwa,” amesema.
CAG Kichere anapendekeza Wakala wa Barabara kuwasiliana na waathirika wa miradi na kuwapatia hundi zao kwa wakati bila kuchelewa zaidi.