Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Busara kumaliza mgogoro wa SBL, Rahco

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Serikali imesema itatumia busara kumaliza mgogoro uliopo baina ya Mamlaka ya Reli (Rahco) na kiwanda cha Bia cha Serengeti Breweries (SBL) ambacho sehemu kubwa ya eneo lake iliwekewa alama ya X (kubomolewa) miaka miwili iliyopita ili kupisha ujenzi mpya wa njia ya reli.

Hayo yamesemwa leo, Machi 17, na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya alipotembelea kiwanda hicho akiwa ameambatana na kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Manyanya amesema uwekezaji uliofanywa  katika kiwanda hicho ambacho awali kilikuwa cha Serikali kabla ya kubinafsishwa una tija kubwa kwa Serikali na kiwanda kimekua kinalipa kodi kubwa na kwa wakati.

"Ardhi ipo ya kutosha, hivyo tutakaa wizara zote zinazohusika na jambo hili na kupata suluhisho, najua hili halina tatizo, busara itatumika na mambo yataenda vizuri. Huyu mwekezaji yuko ‘Serious’, na nchi hii ipo kwa ajili ya kuangalia maslahi mapana na mchango unaofanywa na wawekezaji hawa,’’ amesema Manyanya.

Mwenyekiti wa kamati ya Bunge, Viwanda , biashara na mazingira, Suleiman Sadick ambaye pia ni Mbunge wa Mvomero amesema mgogoro huo unahitaji kutafutiwa suluhu haraka, kwa sababu unashirikisha wawekezaji wa nje na ndani.

"Wawekezaji hawa tunawakatisha tamaa kwa namna moja au nyingine na nia ya kamati yetu kuja hapa leo ni kuunga mkono juhudi za Rais katika kuelekea Tanzania ya viwanda, kazi yetu kubwa ni kwenda kuishauri Serikali ili tuangalie namna ya kulimaliza jambo hili kwa haraka," amesema Sadick.

Alisema, "Sisi kama Bunge tunaunga mkono hivi viwanda vinavyochangia pato la Taifa na vinavyotoa ajira mbalimbali kwa vijana, hivyo tunahakikisha tunavilinda na kusaidia viendelee kuwepo ili Serikali iendelee kupata mapato yake," amesema.

Ni vyema mgogoro huu ukamalizika mapema bila kuathiri uhusiano wa kibiashara “wawekezaji hawa wametuambia wanazo hati mbili ikiwemo ya eneo lenye mgogoro lakini tulipouliza kuhusu wenzetu wa Rahco hawana hati ya eneo hili," amesema.

Mkurugenzi wa Mawasiliano SBL, John Waiku amesema wanaiomba Serikali iwasaidie kuhakikisha eneo hilo halibomolewi kwani watapoteza ajira nyingi na fursa mbalimbali kwa wakulima.



Chanzo: mwananchi.co.tz