Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bunge latoa maagiza Stamico biashara ya mkaa rafiki

Mkaa Dar Matumizi Bunge latoa maagiza Stamico biashara ya mkaa rafiki

Tue, 28 Mar 2023 Chanzo: mwanachidigital

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeliagiza Shirika la Madini nchini (Stamico) kurahisisha masharti ya uwakala wa mkaa wa rafiki Briquettes kuvutia biashara na kuongeza matumizi ya mkaa huo.

Akizungumza wakati wa shughuli ya kupanda zaidi ya miche 2, 000 ya miti aina mbalimbali mjini Geita, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Judith Kapinga amesema kusambaza na kuuza mkaa huo utapunguza matumizi ya mkaa wa kawaida na hivyo kusaidia uhifadhi wa mazingira.

“Mkaa rafiki unatakiwa kuwafikia wananchi kirahisi kote mijini na vijijini kupunguza matumizi ya mkaa wa kawaida ambayo siyo tu upatikana kwa kukata miti na kuharibu mazingira, bali pia siyo salama kwa afya ya binadamu,” amesema Kapinga

Makamu Mwenyekiti huyo ameishauri teknolojia ya kutengeneza mkaa rafiki kutolewa kwa watu na sekta binafsi kuongeza kiwango cha uzalishaji, usambazaji na matumizi mijini na vijijini kupunguza ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa wa kawaida.

Inakadiriwa kuwa asilimia 70 ya hekari milioni moja ya miti inayokatwa kila mwaka hutumika kuzalisha mkaa ambao ndio chanzo kikuu cha nishati nchini, hali inayotishia nchi kugeuka jangwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala.

“Stamico mna mkaa wa rafiki ambao ni wa bei stahimilivu na unaweza kutumika kupika vitu vingi; nishati hii ni rafiki kwa mazingira na afya kwa sababu umetolewa sumu hatarishi, ni vema bidhaa hii ifikie wengi,” amesema

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameipongeza Stamico kwa kuibua teknolojia ya kuzalisha mkaa mbadala rafiki kwa mazingira akibainisha kuwa hatua itasaidia kuhifadhi mazingira na kupunguza madai kuwa sekta ya madini ni kinara cha uharibifu wa mazingira.

“Nawapongeza Stamico pia kwa mpango wa kuhamasisha upandaji wa miti sehemu mbalimbali nchini kwa lengo la kurejesha uoto wa asili unaotishiwa na tatizo la ukataji miti,” amesema Biteko

Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse amesema taasisi hiyo inalenga kupanda zaidi ya miti 10, 000 sehemu tofauti nchini ikiwemo kwenye vyanzo vya maji na maeneo ya taasisi za umma huku miti 2, 000 ikitarajiwa kupandwa mjini Geita.

Chanzo: mwanachidigital