Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC),limeishauri Serikali kuchukua hatua za kumaliza changamoto za msongamano wa shehena za mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, inayopelekea kukosa mapato ya forodha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Akiwasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za PIC, kuanzia Februari 2022 hadi Januari 2023, leo Jumanne, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerry Silaa, amesema msongamano wa shehena za mizigo unaifanya Bandari ya Dar es Salaam, ishindwe kushindana na Bandari ya Mombasa nchini Kenya na Bandari ya Beira nchini Msumbiji.
“Kumekuwa na changamoto ya msongamano wa shehena za mizigo, kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa Bandari na kukosekana kwa mapato ya forodha kwani wanashindwa kushusha baadhi ya shehena za mizigo, katika Bandari ya Dar Es Salaam,”
“Changamoto hizi zinaisababishia Bandari ya Dar es Salaam kushindwa kushindana na Bandari za karibu yake ikiwemo Bandari ya Mombasa, Kenya na bandari ya Beira iliyopo nchini Msumbiji,” amesema Silaa.
Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Jerry Silaa
Silaa amesema, licha ya upanuzi wa bandari hiyo unaonedelea hivi sasa, hautaweza kumaliza changamoto iliyokuwepo ya wingi wa shehena zinazohudumiwa na nyingine kushinfwa kushushwa kutokana na eneo kuwa dogo na kina kidogo.
Silaa amesema PIC inaishauri Serikali kupitia TPA, imalize changamoto zinazouzia kuanza kufanya kazi kwa Bandari Kavu ya Kwala, ambayo imekamilika kwa asilimia 98.
Pia, amesema PIC inaishauri Serikali kuharakisha mchakato wa ujenzi wa Bandari ya Mbegani-Bagamoyo kwa kutumia mapato ya ndani.
Silaa amesema PIC inaipongeza Serikali kwa kuteua Bodi Mpya ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kufanya mabadiliko katika menejimenti yake, kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa mamlaka hiyo.