Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bunge laitaka TIC itoe mwongozo wa uwekezaji

Df38cf88c7f53f66c1ba0f2e8a055fbb Bunge laitaka TIC itoe mwongozo wa uwekezaji

Thu, 15 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KAMATI ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa, imekitaka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kikamilishe uandaaji wa Mwongozo wa Taifa wa Uwekezaji utakaotoa mwelekeo wa taifa kuhusu uwekezaji.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Humphery Polepole aliyasema hayo bungeni Dodoma jana wakati akisoma maoni ya kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Polepole alielekeza mwongozo huo uwekwe kwenye mtandao ili kuwawezesha wawekezaji kutambua matakwa ya kuzingatia kabla ya kuanza mchakato wa kuomba vibali vinavyohusu uwekezaji nchini.

Nayo Kamati ya Bunge ya Bajeti imeweka mkazo kuhusu uwapo wa ofisi za wabunge majimboni na kuziwekea samani ili kusaidia utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Sillo Baran alisema kwa kuwa suala hilo limekabidhiwa kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-Tamiseni) kwa ajili ya utelekezaji, ni vema Bunge likapata maelezo kuhusu mpango wa serikali wa kukamilisha ujenzi wa ofisi hizo.

Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilisema imebaini kupungua kwa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kutokana na maoteo ya bajeti ya nje ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa haitolewi kwa wakati na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Najma Murtaza Giga alisema hatua ya kupunguza utegemezi wa bajeti ya nje ni sehemu ya utekelezaji wa ushauri wa kamati kwa Ofisi ya Waziri Mkuu iendelee kupunguza utegemezi wa fedha za nje na pia ibuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani pamoja na kuongeza uwezo wa kukusanya maduhuli kwenye taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo.

Wakati huohuo, Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, ilisema msongamano wa wafungwa na mahabusu unaongeza maambukizi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) magerezani.

Mwenyekiti wa kamati, Fatuma Toufiq aliyasema hayo bungeni jana wakati akisoma maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Alisema kamati hiyo inashauri kuwe na hatua za awali za upimaji na kuanzishiwa dawa wanaokutwa na TB ili kupambana na ugonjwa huo.

Toufiq aliwaeleza wabunge kuwa, watu wanaoishi na VVU wanaacha kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU kwa sababu ya umbali kutoka vituo vya kutolea dawa hizo hivyo gharama za usafiri zinakuwa kubwa kwani wengi wao wanaishi maeneo ya pembezoni mwa halmashauri zao.

“Watumiaji wachache ambao ni wakazi walio karibu na maeneo ya upatikanaji wa dawa hizo baadhi yao hutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu makazi yao na mawasiliano yao kutokana na hali iliyopo ya unyanyapaa,” alisema

Chanzo: www.habarileo.co.tz