Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwezi mmoja (sawa na siku 30) kuipelekea mpango kazi wa namna walivyojipanga kukabiliana na hoja za kikaguzi zilizoainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Japhet Hasunga ameyasema hayo jana Alhamisi Agosti 25, 2022 mara baada ya kuchambua ripoti ya CAG kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2021 ya TRA.
Amesema katika uchambuzi wao wamebaini TRA haina mifumo thabiti inayoonana inayowezesha taarifa za mfumo mmoja kuonekana kwenye mfumo mwingine.
Hasunga ambaye pia ni mbunge wa Vwawa, amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha upungufu kwenye ufungaji wa vitabu vya hesabu lakini pia katika utendaji wa majukumu yao.
“TRA tumewapa mwezi mmoja watuletee mpango kazi watakaouandaa wa namna walivyojipanga kukabiliana na hoja zote za kikaguzi ambazo zimebainishwa na CAG ili tuone kama wataweza kulitekeleza hilo,” amesema.
Pia, amesema wameiagiza TRA kuhakikisha mifumo yote ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali inatengenezwa na kurekebisha ili iweze kuonana ifikapo Juni 30, 2023.
Amesema mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani wa TRA hauonani na mifumo minginine ikiwemo wa makusanyo wa forodha.
Amesema mifumo ikiwa haionani, hauwezi ukawa na taarifa ambazo ni timilifu.
“Kwa mfano watu wanaagiza bidhaa kutoka nje ya nchi wanafika pale wanatoza ushuru wa forodha, wanalipia baada ya kulipia ikija huku ndani tunataka kuona zikienda sokoni, zinauzwa na zinalipa kodi ya mapato na VAT,”amesema.
Amesema inachotaka kamati ni kuhakisha bidhaa hizo zinafanyaje katika mfumo wa ndani na kwamba mifumo isipoonana inashindikana kuelewa kama kilichoingia kiliweza kulipa kodi za ndani ama hazikufanya vizuri.
Aidha, Hasunga amesema kamati hiyo iliyoanza vikao vyake leo jijini Dodoma ilifanya uchambuzi wa hesabu za Wakala wa Usalama Mahali Pa Kazi (OSHA) kwa mwaka unaoishia Juni 30,2021.
Amesema walibaini kuna mapungufu kidogo katika utayarishaji wa hesabu zao kwa vitabu wanavyowasilisha mara ya kwanza vina makosa ya kiuhasibu.