Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bucha za nyamapori bado zinasuasua

48378d348acda4c543e82d66bc58d6ab Bucha za nyamapori bado zinasuasua

Wed, 17 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WALIOPEWA vibali vya kuanzisha bucha za kuuza kitoweo cha wanyamapori nchini Agosti mwaka jana, bado wanasuasua kwa kushindwa kuanza kufanya uwindaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo changamoto ya kupewa maeneo yasiyo na wanyama.

Katibu wa Wenye Mabucha Tanzania, Mchungaji Emmanuel Absalom, alisema katika mazungumzo na HabariLEO kuwa, waliopewa vibali nchini ni 46, lakini kati yao hakuna aliyefanikiwa kuwinda kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo ya kupewa maeneo yasiyo na wanyama.

Kwa mujibu wa Absalom, waliopewa vibali wameingia gharama kubwa hadi kupewa vibali ikiwemo kuhakikisha wanapata leseni kutoka halmashauri husika ambayo ni Sh 85,500, kupata usajili wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Sh 100,000, kupata kibali kutoka bodi ya nyama Sh 100,000 na upimaji afya Sh 5,000 kwa kila mfanyakazi.

Alizitaja gharama nyingine kuwa ni pamoja na Sh 650,000 kwa ajili ya kununua gogo la kukatia nyama, vibebeo sita vya nyama kila kimoja kikigharimu Sh 45,000, mashine ya kukatia nyama Sh 2,500,000, mashine ya kutolea risiti za kielektroniki (EFD) Sh 550,000, kibali cha kuwinda kwa miaka mitano Sh 295,000, pamoja na kulipa kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kulingana na andiko walilopeleka katika Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa).

Alisema kwa mwenye duka la kuuzia kitoweo cha wanyamapori katika maeneo ya Kwa Mrombo, baada ya kupewa vibali na kukodi silaha ya uwindaji Sh 200,000, gari la kuhifadhia wanyama watakaowindwa (jokofu) ni Sh 400,000, lwalipokwenda kuwinda walikuta maeneo waliyopewa hayana wanyama.

Maeneo hayo alisema ni pa moja na Talamai, Kiteto, Kitwai, Simanjiro, Ipemba, Mpazi, Sikonge mkoani Tabora, Simbaguru Manyoni, Ugala Ninsi na Katavi ambapo kuna vitalu vitatu vya uwindaji.

Alisema maeneo mengine waliyopewa kama Ugala, Kilwa na Kisarawe ndiko kuna wanyama, lakini mvua zinanyesha.

Alisema Januari 27 hadi 29, mwaka huu walikutana na uongozi wa Tawa jijini Arusha na kukubaliana kuanzisha maeneo mapya 20 ya uwindaji, lakini hadi sasa hawajui kinachoendelea.

“Sasa licha ya gharama hizo, wananchi wanaohitaji kitoweo hiki wanasema kama nyama hazipatikani ni heri tufunge mabucha hayo kwani wanataka nyamapori, lakini buchani hakuna,” alisema.

Hivi karibuni Tawa ilikutana na wenye mabucha ya nyamapori na kusisitiza umuhimu wa kuanzishwa mashamba ya kufuga wanyama kwa ajili ya kitoweo ili kuwezesha nyama hizo kuliwa mara kwa mara.

Msimamizi wa Mabucha Tanzania Kutoka TAWA, Gregory Kalokola, alisema kwa simu kuwa, malalamiko ya wenye mabucha na hasara waliyopata, waliyazungumza katika kikao hicho na kukubaliana kuyafikisha kwa waziri mwenye dhamana.

"Hadi sasa tunasubiri majibu kutoka kwa waziri hivyo, niwaombe wenye mabucha wavute subira,” alisema Kalokola.

Kwa mujibu wa Kalokola, ili waziri mwenye dhamana atoe vibali, lazima kwanza atume timu za wataalamu kutembelea maeneo hayo kujiridhisha kama yana wanyamapori na kujiridhisha kuwa hakuna migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Chanzo: habarileo.co.tz