Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Brela yawataka wananchi kurasimisha biashara mazao ya kilimo

Btela Mazao Kilimo.jpeg Brela yawataka wananchi kurasimisha biashara mazao ya kilimo

Tue, 29 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wafanyabiashara wa mazao ya kilimo nje ya nchi mkoani Kilimanjaro, kurasimisha biashara zao kama serikali ilivyoelekeza, hatua ambayo itawawezesha kulindwa kisheria na kuondoa usumbufu ambao wamekuwa wakiupata katika maeneo ya mipakani. Rai hiyo imetolewa leo Jumatatu, Agosti 28, 2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Majina ya Biashara na Makampuni Brela, Isdor Nkindi wakati wa utoaji wa mafunzo kwa wauzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi, Mkoa wa Kilimanjaro. Mafunzo hayo ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji kutaka wafanyabiashara hao wasaidiwe kutambua taratibu, kanuni za kazi zao ili kuondoa usumbufu.

Nkindi amesema hivi karibuni serikali ilitoa maelekezo ya uzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi na kueleza kuwa haijakataza mtu yeyote kufanya biashara ya mazao hayo nje, ila kinachohitajika ni kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ikiwemo kurasimisha biashara.

Aidha amesema wafanyabiashara wengi, hawana uelewa juu ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uuzaji wa mazao nje ya Nchi, hali ambayo imekuwa ikiibua changamoto na vikwazo katika maeneo ya mipakani wakati wa usafirishaji wa mazao, hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa na kuboresha mazingira yao ya biashara. "Kikubwa wafanyabiashara kabla ya kuanza biashara ya nje wanapaswa kufahamu taratibu zilizopo na wanatakiwa kurasimisha biashara zao brela ili kuweza kulindwa kisheria na kuondoa usumbufu," amesema. Ameongeza kuwa, "Changamoto kubwa ni kwamba wafanyabiashara wengi wanapata shida kuzielewa na kuzitumia taratibu zilizoko, kwani sheria taratibu na miongozo ya usafirishaji na uuzaji mazao ya kilimo nje zipo, ila wafanyabiashara walikuwa wanapata changamoto ya kusafirisha kwa kuwa hawakuzifuata," amesema. Nkindi amesema katika mafunzo hayo, pia Brela itajifunza kwa wafanyabiashara ni maeneo gani ambayo watahitaji siku za usoni kujengewa uwezo zaidi au kuwekewa miongozo na taratibu rafiki zaidi ili kuweza kufanya biashara zao bila usumbufu kwani lengo la biashara ni kutafuta faida na kutoa huduma kwa walengwa. Zuberi Hamisi ambaye ni mfanyabiashara wa nafaka Nchi jirani ya Kenya kupitia mpaka wa Holili, amesema awali walikuwa na vibali vya kusafirisha mazao lakini baadaye Serikali ilisema havikidhi mahitaji ya usafirishaji wa mazao nje na kutakiwa kukata vingine hali ambayo iliibua malumbano baina ya wafanyabiashara na serikali. "Mtakumbuka hapo nyuma kidogo kulitokea malumbano baina yetu wafanyabiashara na serikali, tukiambiwa hatuna vibali vya kusafirisha mahindi kwenda nje ya nchi, ilihali vilikuwepo vile vya mwanzo na hii ilisababisha tukatozwa faini ya Sh800,000 ambayo mimi binafsi inaniuma mpaka leo," amesema. Amesema ipo haja serikali kuwa karibu na wafanyabiashara na kuwafanya marafiki, ili waweze kupeleka mawazo yao wakae mezani na kujadiliana namna bora ya biashara ya mazao ya kilimo nje ya nchi. Julieth John ameishauri serikali kuondoa urasimu na vikwazo vya kupeleka mazao nje nchi, ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kupata masoko ya nje. "Kutokana na kwamba kwa sasa tumepata neema ya mavuno, Serikali inunue mahindi kwa bei nzuri, ili wafanyabiashara na wakulima wafaidike, pia kuna figisu za kusafirisha mazao nje, serikali iondoe vikwazo, maana vikwazo vimekuwa vikisababisha nchi nyingine zenye chakula kutumia fursa hiyo kupeleka mazao kule kwenye upungufu," amesema John.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live