Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imefungua kambi maalum ya kukutana na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo nje ya nchi ili kuwapa mbinu za namna ya kurasimisha biashara zao ili zitambulike na wafanye kazi ya usafirishaji kwa kufuata sheria. Kambi hiyo ya siku tatu iliyoanza Agosti 24 hadi 26, 2023 na kuwatanisha wafanyabiashara zaidi ya 150, ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji kutaka wafanyabiashara hao wasaidiwe kutambua taratibu, kanuni za kazi zao ili wasisumbuliwe. Akizungumzia hayo, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) , Isdor Nkindi amesema kambi hiyo inaenda sambamba na mafunzo kwa wafanyabiashara wa mazao nje ya nchi ili waelewe umuhimu wa kurasimisha biashara zao na kupata leseni sambamba na kufahamu kanuni na taratibu zake.
“Lengo letu mfaye kazi kwa uhuru hivyo changamkieni fursa za kujikwamua kiuchumi ikiwemo kufanya biashara kwa urahisi kutokana na usajili wenu na sasa tupo hapa tumeweka kambi kwaajili ya usajili wa biashara zenu ili mfungue masoko ya biashara kwasababu mtatambulika kisheria na kufurahia maisha,” amesema. Akizungumzia mafunzo hayo Katibu Tawala Msaidizi, Ramadhani Mdeleka alisema mafunzo hayo yametolewa kwa wafanyabiashara kwaajili ya kufuata sheria ya kuwasaidia kufuata sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji mazao nje ya nchi hasa mpaka wa Namanga ili kuondokana na usumbufu wanaoupata na kuangushia Serikali lawama.
"Anzeni kutumia mafunzo haya kufuata taratibu zote za kisheria ikiwemo usajili na upataji leseni wa biashara zao, ili zitambulike rasmi na kuepuka usumbufu huko mipakani na kuangushia Serikali lawama". Mmoja wa wafanya biashara wanufaika wa mafunzo hayo, Agnes Mushi alisema walikuwa wanahofia kurasimisha biashara zao kwa hofu ya kuhesabiwa kiwango kikubwa cha kodi. "Hofu yetu ndio umaskini wetu, maana fedha tunazotumia kuhonga huko mipakani ili kuvunja sheria za biashara zetu, kumbe ni kubwa tofauti na kurasimisha hivyo kuanzia sasa tumeelewa na tuko tiyari kufuata kanuni na taratibu zote ili kuondokana na usumbufu mkubwa tuliokuwa tunakumbana nao," amesema.