Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi Vodacom azungumzia bei ya bando

Basi Vodacommpicc Mkurugenzi wa Vodacom akifanya mahojiano

Tue, 25 Jan 2022 Chanzo: mwananchi

Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Sitholizwe Mdlalose amesema kampuni za mawasiliano nchini hazipati faida jambo linaloweza kukwamisha uwekezaji.

Mdlalose alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu kuhusu ujumuishaji watu kwenye fursa za kidijtali, mazungumzo yaliyorushwa mbashara kupitia majukwa ya kielektroniki ya MCL.

“Soko la Tanzania lina changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi. Sekta inakabiliwa na changamoto ya kukosa faida jambo ambalo linaloweza kupoteza mvuto kwa wawekezaji,” alisema Mdlalose.

Ingawa bei ya kifurushi cha intaneti nchini ni ndogo ikilinganishwa na mataifa mengine lakini kampuni za simu zinatumia gharama kubwa kuzalisha na kufikisha huduma kwa mteja hivyo uendelevu katika biashara unakosekana.

“Kuna mazungumzo yanaendelea kati ya wadau na Serikali kuangalia gharama za uzalishaji data na masuala ya kodi ambayo ni zaidi ya asilimia 30 nchini wakati katika masoko mengine kama Ulaya ni asilimia 21,” alisema Mdlalose.

Alisema dhumuni la Vodacom ni kuwaunganisha Watanzania wote katika ulimwengu wa kidijitali wakiwamo wakulima kwa kuwaonyesha masoko ya ulimwengu na wanafunzi kusoma kidijitali.

“Vodacom sasa tunabadilika kutoka kampuni ya huduma za simu (telecom) kuwa ya huduma za kiteknolojia (techcom) kwa wakati wote tumefanya yale tunayopaswa kufanya. Hivi sasa teknolojia inakuwa kwa kasi na sisi tunaendelea kuangalia namna ya kuboresha maisha ya Watanzania,” alisema.

Akijibu swali la Machumu kuhusu mapinduzi ya dijiti alisema kuna hofu kuwa inakwenda kumaliza kazi za watu lakini uhalisia ni kwamba inatoa fursa nyingi zaidi. Alisema ubunifu wa kidijitali unapaswa kukuzwa kwa kuondolewa au kukingwa na vihatarishi (risk) vilivyopo.

Kuhusu kuongeza upatikanaji wa intaneti hadi kuwafikia asilimia 80 ya Watanzania, Mdlalose alisema jambo hilo litafanikishwa na iwapo upatikanaji wa vifaa vyenye uwezo wa 3G na 4G utaongezeka.

Alhamisi wiki hii, MCL kwa kushirikiana na Vodacom watafanya kongamano kuhusu kuunganishwa kwa watu kidijitali na kuwakutanisha wadau wa sekta ya mawasiliano nchini. Huo ni mwendelezo wa mijadala ya Jukwaa la Fikra (MTLF).

Chanzo: mwananchi