Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Edwin Rutageruka amezitaka taasisi zinazofanya kazi moja kwa moja na wafanyabiashara kubadili mtazamo katika utendaji ili kuziba mianya ya rushwa.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 3, 2019 ikiwa ni siku maalum ya kupinga rushwa inayoadhimishwa kwenye maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Amesema ukiritimba, kuzungushana na wafanyabiashara kunafungua mianya ya rushwa, ili kuepuka hilo ametaka kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi.
"Niombe taasisi zote za biashara zibadilishe mitazamo ziweke mazingira mazuri ya biashara kuwasaidia wafanyabiashara na wawekezaji,” amesema.
Rutageruka pia alitoa rai ya elimu ya kutopokea rushwa iliyokuwa ikitamkwa na wanafunzi miaka ya nyuma kabla ya kuwasalimu walimu wanapoingia darasani, kurejeshwa ili kuwajenga watoto kukataa rushwa.
"Ili nchi iendelee inahitaji kupiga vita vitu vitatu maradhi, umasikini na ujinga, sitoomba wala sitopokea rushwa,” amesema Rutageruka.