Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi Tantrade aeleza upekee wa mwanamke kiongozi

418b3f0563c9fac4e1a98370f20178eb Bosi Tantrade aeleza upekee wa mwanamke kiongozi

Fri, 16 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NAIBU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis amesema mwanamke kiongozi hufanya kazi nyingi nje ya cheo chake ikiwa ni pamoja na kushauri, kusuluhisha na kuokoa wale walio hatarini kupotea.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kuhusu nafasi ya mwanamke katika uongozi.

Latifa alisema si rahisi kutenganisha nafasi ya mama katika cheo cha mtumishi mwanamke kiongozi katika taasisi au eneo analolizimamia au kuongoza.

“Nafasi ya mama ni ngumu kuitenganisha katika nafasi ya kiongozi mwanamke kwenye taasisi au idara anayoiongoza, kwanza jambo kubwa na la msingi ni kwamba mwanamke kiongozi hufanya kazi zaidi kuliko kiongozi mwanaume,” alisema Latifa.

Alisema katika taasisi, shirika, idara au hata nafasi ya Rais kuna wakati mamlaka ya cheo hicho hugeuka eneo la usuluhishi kwa watumishi wengine kwa sababu mwanamke anaweza kulibeba jambo na kulitafutia suluhu hivyo kuponya roho za watumishi.

“Wakati mwingine unatekeleza majukumu yako alafu unafuatwa na walio chini yako au unaona utendaji wa fulani umeshuka na hayuko sawa inabidi umsikilize na wengi tumewaponya wamebadilika na kurudi kwenye njia salama, hiyo ni kwa sababu mama hawezi ona mtoto anaharibika, atatumia kila mbinu kumsaidia abadilike,” alisema Latifa.

Alisema wanawake wengi viongozi pamoja na kutekeleza majukumu yao lakini pia wamekuwa msaada mkubwa wa kuponya roho na kuwa washauri na wasuluhishi wa migogoro ya watumishi.

“Mara nyingi katika nafasi za uongozi sio viongozi wote wanaweza kugundua kama mtumishi fulani ana tatizo, hivyo utendaji wake umeshuka kwa kuwa anapitia magumu. Ila mimi mama nikimuangalia tu usoni na ukiona ripoti anayokuletea unagundua kuna tatizo, unamwita unaketi naye unampa nafasi anaeleza yanayomsibu, unamshauri anarudi kwenye hali ya kawaida na utendaji kazi unapanda, hicho ni kipawa cha mwanamke,” alisema Latifa.

Alisema kama ilivyo nyumbani wakati mwingine hakuna chakula, lakini mama huweza kujiongeza na kubuni njia ya kupata chakula na kikapatikana na familia haitalala njaa, ndivyo pia ilivyo kwenye nafasi za uongozi mwanamke hutumia ubunifu kuifanya taasisi au kampuni kukua kwa ubunifu.

Akizungumzia nafasi yake, Latifa alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaunganisha kimasoko nje ya nchi wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania.

Alisema mazao kama soya, parachichi, pilipili, viungo, samaki na bidhaa nyingine zimepata soko katika nchi mbali mbali ikiwemo bara la Ulaya, Asia na Marekani na kwamba hiyo ni juhudi ya Tantrade kutafuta masoko nje ya nchi.

“Hivi karibuni tumepata soko nchi ya Falme za Uarabuni, kupeleka samaki na parachichi na pia nchi nyingine za Asia kama China, tuna soko la soya na bidhaa nyingine na hayo yote ni juhudi za Tantrade za kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania nje,” alisema Latifa.

Akizungumzia maandalizi ya Maonesho ya 45 Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DIFT) yanayotarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13, mwaka huu, Latifa alisema yanaendelea na kwamba wanatumia balozi za Tanzania kuyatangaza na kupata washiriki wa nje na mwitikio ni mzuri.

Chanzo: www.habarileo.co.tz