Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi ATCL: Hatukwenda Afrika Kusini kula keki bali kuzindua ruti mpya

65297 Pic+atcl

Wed, 3 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limefafanua kukosekana kwa mawasiliano miongoni mwa maofisa wa Uwanja wa Ndege wa O.R.Tambo kama moja ya changamoto zilizojitokeza katika ufunguzi wa safari zake kwenda Afrika Kusini.

Ijumaa iliyopita, shirika hilo lilianza kurusha ndege yake ya Airbus 220-300 kwenda Johannesburg lakini halikufanikiwa kufanya sherehe ya ufunguzi wa ruti hiyo kama ilivyokuwa imepangwa.

Taarifa za kwenye mitandao ya kijamii zilidai kuwa kutopokelewa kwa ugeni wa ATCL ni vita ya kibiashara kwa sababu ATCL sasa imekuwa ni mshindani katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Hata hivyo akizungumza na Mwananchi jana, mkurugenzi mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alikana madai hayo huku akieleza kwamba hakukuwa na mawasiliano mazuri upande wa Afrika Kusini na kwamba hawakwenda nchini humo kula keki ila kuzindua ruti mpya.

Alifafanua mkasa huo kwa kuhusisha na kutopokelewa ugeni wa ATCL na mkanganyiko uliokuwepo kati ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Afrika Kusini (ACSA) na maofisa wa uhamiaji nchini humo.

Alisema kwamba maofisa uhamiaji hawakupewa taarifa na ACSA kuhusu ujio wa ndege ya ATCL.

Pia Soma

“Nadhani ACSA hawakutilia maanani suala hilo wakidhani kwamba watu wa uhamiaji walipewa taarifa na kampuni ya Swissport ambayo ndiyo iliyotupokea na kutupatia huduma baada ya kutua uwanjani,” alisema Matindi.

“Lakini tuseme ukweli, kampuni inayotoa huduma uwanjani haina mamlaka ya kuitaarifu idara ya uhamiaji.”

Alisema ndio maana baada ya kuwasili eneo la uhamiaji uwanjani hapo, abiria waliowasili na ndege ya ATCL hawakuruhusiwa kuingia katika jengo la abiria wanaowasili.

“Kutokana na ukweli kwamba hakukuwa na mawasiliano mazuri, ilikuwa ni sahihi kwa maofisa uhamiaji wa Afrika Kusini kufanya vile. Hatuwalaumu kwa sababu tunajua ni kwa sababu za kiusalama,” alisema mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, Matindi alisema tatizo hilo lilitatuliwa baada ya dakika 30, na ofisa mwandamizi alikwenda kuwachukua ili waelekee kwenye ukumbi wa sherehe za ufunguzi.

Alisema alimpigia simu kaimu balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kumuomba radhi kwamba wasingeweza kwenda kwenye sherehe kwa sababu muda haukuwa rafiki kwao.

Mbali na kaimu balozi, waliokuwepo kwenye sherehe hizo ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa ACSA na maofisa wengine waandamizi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Ili kutowavunja moyo wateja wao, Matindi alisema hawakutaka kuchelewa kuanza safari ya Dar kwa kisingizio cha sherehe za ufunguzi. “Hatukwenda Afrika Kusini kula keki bali kuzindua ruti yetu mpya ambayo ni soko muhimu sana kwa utalii,” alisema.

ATCL inauza tiketi ya kwenda na kurudi Afrika Kusini kwa bei ya ofa ya Dola za Marekani 299 (sawa na Sh687,700) ambayo itafikia ukomo Julai 15 mwaka huu, itakuwa na safari nne kwa wiki; Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi.

Bei ya kawaida itakayotozwa kwa safari hiyo ni Dola 347 (sawa na Sh798,100).

Matindi alisema ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 130, siku hiyo ilibeba abiria 91 ambapo alisema ni mafanikio makubwa kwa safari ya kwanza ya ruti mpya.

Chanzo: mwananchi.co.tz