Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bonge la Mpango yawaingizia Mil 60/- wateja wa NMB

Fcd29b5ea77e14d3e6e6526e96bcfc9a Bonge la Mpango yawaingizia Mil 60/- wateja wa NMB

Sun, 25 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BENKI ya NMB imeshatoa zawadi zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 60 kuzawadia washindi wa promosheni ya Bonge la Mpango inayohamasisha utamaduni wa Watanzania kujiwekea akiba benki.

Hayo yamebainishwa juzi na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi ya pikipiki ya miguu mitatu kwa mshindi Paulina Mushi, mkazi wa wilayani Mbulu Mkoa wa Manyara.

Mlozi alisema mpaka sasa benki hiyo imeshakabidhi zawadi za kampeni ya Bonge la Mpango zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 60 kwa washindi wa maeneo mbalimbali nchini.

Meneja Uhusiano wa Amana za Wateja wa NMB Makao Makuu, Monica Job alisema wateja walioshinda katika kampeni hiyo wanatoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Tanga, Mwanza, Manyara, Tabora, Morogoro na Pwani.

Nsolo alieleza kwamba bahati nasibu ya benki hiyo ilianza mwanzoni mwa Februari mwaka huu ikilenga kujenga tabia ya wananchi kujiwekea akiba pamoja na kurudisha kiasi cha fedha kwa wananchi.

Alizitaja baadhi ya zawadi zinazoshindaniwa kuwa ni fedha taslimu ambapo watu 10 kila wiki wanajishindia hadi Sh 500,000, pikipiki ya miguu mitatu mbili kila wiki, gari dogo la kubeba mizigo aina ya kilikuu kila mwezi na gari la kifahari aina ya Toyota Fortuner ambavyo vyote hadi bahati nasibu hiyo inamalizika zitatumia zaidi ya Sh milioni 550.

Mshindi wa pikipiki ya magurudumu matatu, Paulina Moshi aliishukuru NMB kwa zawadi hiyo iliyompatia.

“Mimi hapa ni mjane, mume wangu amefariki, leo anatimizi siku 55 tangu kifo chake, naona Mungu kupitia NMB ameona unyonge wangu na kunipatia zawadi hii itakayosaidia kuingiza kipato cha familia yangu, Mungu awabariki sana benki hii,” alisema mkazi huyo wa Mbulu.

Alisema anakumbuka ilikuwa Machi 17, mwaka huu alipigiwa simu na mtu kutoka NMB akimjulisha ameshinda zawadi kupitia Bonge la Mpango, lakini hakuamini mpaka alipofika kwenye tawi Mbulu kuhakikishiwa ni kweli.

Pia alisema hakufahamu kuhusu kampeni hiyo lakini alikuwa na utaratibu wa kuweka fedha kwenye akaunti yake hivyo ushindi huo hauna upendeleo na wengine waendelee kuweka fedha na kufungua akauti mpya watajishindia zawadi hizo.

Aliongeza kuwa hakutegemea kuona upendo aliooneshwa na wafanyakazi wa NMB kwa kuwajali mpaka pikipiki hiyo kufikishwa nyumbani kwake eneo la Mtaa wa Ujenzi katika Halmashauri ya Mbulu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz