AGIZO la Rais Samia Suluhu Hassan kwa wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuwapanga vyema wafanyabiashara wadogo, maarufu machinga, limeanza kutekelezwa jijini Dar es Salaam kwa kuondoa vibanda vilivyopo maeneo ya karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Juzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, aliagiza vibanda vya biashara vilivyoko pembezoni mwa barabara viondolewe.
Katika kutekeleza agizo hilo, jana Nipashe ilishuhudiwa vibanda vilivyokuwa maeneo ya kuanzia uwanja huo wa ndege hadi TAZARA vikiwa vimebolewa, mashuhuda wakidai kuwa ubomoaji ulifanyika usiku wa kuamkia jana.
Nipashe ilishuhudia baadhi ya wafanyabiashara wakiwa wanachukua baadhi ya bidhaa zao zilizoharibiwa katika utekelezaji wa agizo hilo.
Septemba 13, mwaka huu, Rais Samia aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuchukua hatua za kuwapanga vyema machinga na kwamba hataki kuona anayoona kwenye televisheni ya kupigana, kuchafuana na vitu kumwagwa.
Wakati Rais akitoa agizo hilo, Septemba 9 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makalla alikuwa ameshapiga marufuku ufanyaji wa biashara kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara zote za mkoa huo baada ya utaratibu huo kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani na ongezeko la ajali.
Rais Samia aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya wakati wanachukua hatua ya kuwapanga machinga, wahakikishe hawasababishi vurugu, fujo na uonevu na kuwataka machinga nao wafuate sheria na kanuni zilizopo na kutii wanayopangiwa na viongozi hao wakiwamo wa wakuu wa wilaya.
Akizungumza katika Soko la Kariakoo, Makalla ambaye alilitembelea baada ya kuzuka ugomvi wa wafanyabiashara na mmoja wao kuvua nguo zote wakati wakigombea maeneo ya biashara, aliwaagiza wakuu wa wilaya kuainisha maeneo ambako watawapeleka.
Makalla alisema uchunguzi umebaini kuwapo kwa kero zinazosababishwa na ufanyaji biashara holela kwenye maeneo ya watembea kwa miguu na hifadhi za barabara.