Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Boeing 787-8 Dreamliner ‘Hapa Kazi Tu’ usipime

10753 Ndege+pic TanzaniaWeb

Thu, 5 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyoagizwa na Serikali imeanza kupamba kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, huku mabango kadhaa jijini Dar es Salaam yakiikaribisha katika anga la Tanzania.

Ndege hiyo bado haijatua nchini, lakini duru zinasema wakati wowote mwezi huu itaanza kupeperusha bendera ya Tanzania angani ikitoa huduma za usafiri za ndani na nje ya nchi.

Kuingia kwa ndege hiyo kubwa kutalifanya Taifa kuwa na ndege mpya nne zilizonunuliwa tangu Rais John Magufuli aingie madarakani.

Ndege nyingine ambazo tayari ziko nchini na zinafanya safari ni Bombardier Q400 tatu ambazo zinasafirisha abiria ndani na nje ya nchi zikiwa chini ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

Ndege hizo kila moja ina uwezo wa kuchukua abiria 76, lakini Dreamliner inayokuja ina uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 242 wakiwa katika madaraja matatu yenye hadhi za juu.

Kuanzia mwaka 2011, ATCL imekuwa ikisuasua huku ikitumia ndege moja aina ya Bombadier kufanya safari zake. Rais Magufuli aliingia madarakani akiwa na mpango wa kuifufua ATCL na kuibuka na mkakati wa kununua ndege sita mpya kati ya mwaka 2016 na 2018.

Kwa mujibu wa Shirika la Boeing linalotengeneza pia Boeing 787-8 Dreamliner, aina hiyo ya ndege ilianza rasmi kufanya kazi mwaka 2011 likitaka kuziondoa kwenye soko ndege zake aina ya 767-200ER na 767-300ER pamoja na kuongeza soko la safari za mbali ambalo ndege kubwa zaidi haziwezi kufanya kazi kwa faida. Dreamliner 787-8 inamiliki robo tatu ya soko la ndege aina ya 787 zinazoagizwa na wateja kutoka shirika hilo.

Ujio wa ndege hiyo nchini utaongeza ushindani wa soko la usafirishaji kwa ndege katika ukanda wa Afrika Mashariki ambalo kwa sasa limetawaliwa na Kenya, Ethiopia na Rwanda.

Kutokana na ujio wa ndege hiyo, hivi sasa ATCL imeanza kuwinda masoko ya Kenya, Burundi, Rwanda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Pia kampuni hiyo inatupia jicho kwenye masoko ya masafa marefu yakiwamo ya Mashariki ya mbali, Mashariki ya kati, Ulaya, Afrika Kusini na Afrika Magharibi.

Chanzo: mwananchi.co.tz