Wakati wakazi wa Halmashauri ya Mlimba Morogoro wakiiomba Serikali kuharakisha maboresho ya barabara zilizoharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini imezitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kutumia fedha za matengenezo ya barabara zilizotolewa na mfuko huo kama ilivyokusudiwa.
Jana Aprili 15, 2024 baada ya kufanyika uchaguzi wa katibu na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Barabara mkoani hapa, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga amesema bodi hiyo itahakikisha inazigawa fedha za matengenezo ya barabara kwa wakati kwa wakala wa barabara pamoja na kuzifuatilia kwa makini kuhakikisha zinakwenda kutimiza yale yaliyokusudiwa.
Kalimbaga amesema hadi kufikia Machi, 2024 Sh110 bilioni zimetolewa kwa Tanroads huku, Sh89 bilioni zikitolewa kwa Tarura kwa ajili ya matengenezo ya barabara nchi nzima.
Amesisitiza kuwa bodi hiyo inaendelea kutoa fedha kwa kadri inayoletewa kutoka Hazina.
"Sisi kama bodi jukumu letu kuu ni kuhakikisha mara tu tunapopata fedha, tunazigawa kwa Tanroads na Tarura na haifiki siku tatu fedha hizo zinakuwa zimefika kwao,” amesema Kalimbaga.
Kuhusu uanzishwaji wa baraza hilo, Kalimbaga amesema watalitumia kuhakikisha wanajadili na kuzifanyia kazi hoja za watumishi pamoja na kuhakikisha motisha na stahiki kwa watumishi zinapatikana ili kuleta ari na kasi ya utendaji kazi wa bodi.
Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara linatarajiwa kuzinduliwa wiki ijayo na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.
Hatua za awali za uzinduzi huo zimefanyika Aprili 15, 2024 mkoani Morogoro kwa kufanya uchaguzi wa katibu na wajumbe wa baraza hilo
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Aprili 16, 2024, mkazi wa Mlimba, Cleophace Audax amesema baada ya mvua kunyesha katika halmashauri hiyo barabara nyingi zimebomoka na nyingine zinapitika kwa tabu jambo linalozorotesha maendeleo ya halmashauri hiyo.
"Mvua kubwa zinazonyesha tangu mwaka jana zimesababisha madaraja na baadhi ya barabara muhimu hapa Mlimba kuharibika vibaya, madaraja nayo yamesombwa na maji, tunaiomba Serikali ihakikishe barabara hizi zinatengenezwa kwa wakati ili Mlimba irudi kama zamani,”amesema.
"Kama mnakumbuka Barabara ya Mlimba Ifakara ndiyo imeongoza kwa kubomoka mara kwa mara na kusababisha mawasiliano ya Ifakara na Mlimba kukatika, hii barabara ndiyo inaongoza kupitisha watu kwenda Halmashauri ya Ifakara na Mlimba sasa mawasiliano yakikosekana kwa muda mrefu maendeleo ya watu nayo yanachelewa,” amesema mkazi huyo.
Mkazi wa Tungi, Manispaa ya Morogoro, Samson Safari amesema barabara ya Tungi-Nanenane yenye urefu wa kilometa nne ya vumbi inatakiwa kukarabatiwa maana mvua ikinyesha inapitika kwa shida.
"Hii babarara ya Tungi-Nanenane ina jumla ya kilometa nne, awali ilikuwa korofi na ilipitika kwa shida lakini baadaye Serikali ikaleta greda kwa ajili ya kuipanua na kuitengeneza, sasa yapata miezi miwili baada ya greda kupita, mvua ikinyesha kidogo tu barabara haipitiki,” amesema Safari.